Kwingineko

Teknolojia juu ya teknolojia EPL

ENGLAND:VIONGOZI wa Ligi kuu ya England wanatarajia kuingiza teknolojia mpya ya Semi-Automated Offside Technology (SAOT) ambayo itaunganishwa na ile ya usaidizi wa muamuzi kwa njia ya video VAR ili kung’amua kwa urahisi matukio ya offside kwenye ligi hiyo mwishoni mwa msimu huu au mapema msimu ujao.

Vyombo vya habari nchini England vimeripoti kuwa hatua hii inakuja baada ya viongozi hao kuichunguza kwa makini teknolojia hiyo ikiwemo majaribio na kujiridhisha kuwa inaweza kupunguza makosa na muda wa kufanya maamuzi ya sheria hiyo tata zaidi kwenye sheria 17 za soka.

Mkurugenzi wa mpira wa miguu wa ligi hiyo Tony Scholes, alikiri kuwa na mashaka na teknolojia hiyo lakini kupitia majaribio pamoja na kuangalia matumizi yake kwenye kombe la Carabao wamejiridhisha kuwa ni sahihi na ni wakati mzuri sasa wa SAOT kutumika kwenye ligi hiyo.

“Lazima nikiri kuwa kulikuwa na ugumu wa kufanya maamuzi juu ya hili, hatukuwa na uhakika wake. Lakini kwa maendeleo yaliyopatikana katika miezi hii mitatu minne ya majaribio hivi karibuni tunaamini tunaleta mfumo mzuri sana kwa ligi yetu” amesema Scholes

Pamoja na hayo Premier League pia inatarajia kuanza kutangaza maamuzi ya mwamuzi wa VAR kwa mashabiki uwanjani mapema mwanzoni mwa msimu ujao, lengo likiwa ni kuwafanya mashabiki walio viwanjani kujua maamuzi ya VAR. Teknolojia hiyo ilitumika kwenye kombe la dunia 2022 nchini Qatar na inatumika kwenye baadhi ya ligi za Ulaya ikiwemo Laliga

Related Articles

Back to top button