Africa

Tanzania yapanda nafasi tatu Fifa

TANZANIA imepanda nafasi tatu katika viwango vya ubora wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mwezi Septemba.

Huenda matokeo mazuri iliyopata katika michezo miwili ya kufuzu fainali za Afrika (Afcon) dhidi ya Ethiopia na Guinea yamechangia. Mchezo wa kundi H wa kwanza dhidi ya Ethiopia ilipata sare tasa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na dhidi ya Guinea ugenini mabao 2-1 nchini Ivory Coast.

Kwa mujibu wa viwango hivyo, Tanzania imepanda hadi nafasi ya 110 kutoka ya 113 ya mwezi Julai.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki Uganda inaongoza ikipanda nafasi tano kutoka 95 hadi 90, ikifuatiwa na Kenya iliyopanda nafasi sita kutoka 108 hadi 102, ikifuatiwa na Tanzania, Rwanda ikipanda nafasi moja kutoka 131 hadi 130, Burundi ikipanda nafasi tatu kutoka 139 hadi 136, Ethiopia ikishuka nafasi mbili kutoka 143 hadi 145.

Timu zinazoongoza Afrika ni Morocco katika nafasi ya 14 ikifuatiwa na Senegal imeshuka nafasi mbili 19 hadi 21, Misri ikipanda nafasi tano kutoka 36 hadi 31, Tunisia imepanda nafasi tano kutoka 41 hadi 36, Nigeria ya 39 na Algeria ikipanda nafasi tano 46 hadi 41.

Kidunia Argentina inashika usukani ikifuatiwa na Ufaransa, Hispania, England na Brazil.

Timu iliyopanda kwa pointi nyingi ni Brunei pointi saba kutoka 190 hadi 183 huku Qatar ikishuka kwa pointi nyingi yaani 10 kutoka 34 hadi 44.
Mwisho

Related Articles

Back to top button