Burudani

Tanzania kupanua utambuzi wa ujuzi sekta bunifu

MOROGORO: TANZANIA imeanza rasmi mchakato wa kupanua mfumo wa utambuzi wa ujuzi nje ya elimu rasmi ili kuwanufaisha vijana na wanawake wanaojihusiha kwenye sekta ya utamaduni na ubunifu.

Hatua hiyo inalenga kuwatoa vijana katika ajira zisizo rasmi na kuwaingiza katika ajira zenye staha na ulinzi wa kisheria.

Mchakato huo, uliyowakutanisha wawakilishi 42 kutoka wizara zinazoshughulikia kazi na ajira, mashirika ya waajiri na wafanyakazi, vyama vya sekta ya ubunifu, taasisi za mafunzo pamoja na mamlaka za uthibitishaji wa sifa.

Warsha hiyo imeandaliwa na International Labour Organization (ILO) kupitia mpango wa Global Skills kwa ufadhili wa Serikali ya Norway.

Akizungumza na Spoti leo, Hafidh Khamis, Ofisa wa Programu wa ILO, amesema lengo la kupanua mfumo wa kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (Recognition of Prior Learning – RPL) ni kuhakikisha vijana wanaofanya kazi katika sekta ya ubunifu wanapata utambuzi rasmi wa ujuzi wao.

“Sekta ya utamaduni na ubunifu inakua kwa kasi na inachangia ajira na kipato. Tunataka kuona vipaji vya vijana vinatambuliwa rasmi ili viwape fursa bora zaidi za ajira, mikataba na ujasiriamali,” amesema.

Kiini cha warsha hiyo ni kuupanua mfumo huo katika uchumi wa utamaduni na ubunifu unaojumuisha muziki, filamu, sanaa za maonesho, kazi za mikono, mitindo, uchapishaji na ubunifu wa kidijitali.

Kwa upande wake, Witness Siöbjorn, mwanamuziki wa Bongo Fleva na Rais wa Tanzania Musicians Union (TAMUFO), amesema kwa muda mrefu wasanii wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa kutegemea uzoefu bila kutambuliwa rasmi na mifumo ya kisekta.
“Nina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 kwenye sanaa.

Zipo changamoto nyingi nimepambana nazo hadi kufika hapa nilipo na bado hata sasa, wakati sanaa imekuwa ajira, changamoto hizo bado zipo. Vijana wanakosa mifumo rasmi inayotambua ujuzi wao. Mfumo huu utatusaidia kupata hadhi na kuaminika zaidi katika soko la ajira,” amesema Witness.

Naye Mrisho Mrisho, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Masoko wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), amesema wanawake ni sehemu kubwa ya nguvu kazi katika sekta ya ubunifu, hasa katika kazi za mikono, mitindo na sanaa za maonesho, lakini wanakabiliwa na changamoto za mafunzo rasmi, mitaji na masoko.

Amesema kupitia upanuzi wa RPL unaozingatia usawa wa kijinsia, wanawake wataongezewa fursa ya kupata utambuzi wa ujuzi, kushiriki katika masoko yenye thamani kubwa na kupata ajira zenye staha.

Kwa upande wake, Dk. Kassim Kapalata, Mkurugenzi wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi wa Trade Union Congress of Tanzania (TUCTA), amesema sehemu kubwa ya vijana katika sekta ya ubunifu wanafanya kazi katika mazingira yasiyo rasmi bila mikataba wala hifadhi ya jamii. Amesisitiza umuhimu wa kujiunga na mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi ili kulinda haki zao.

“Utambuzi wa ujuzi ni daraja muhimu la kuwavusha vijana kutoka sekta isiyo rasmi kwenda kwenye ajira rasmi na endelevu. Nawashauri vijana wenye vipaji kujiunga katika mashirikisho mbalimbali ya vyama vya wafanyakazi ili wawe na sehemu ya kupazia sauti zao na hatimaye kupata haki zao,” amesema Dk. Kapalata.

Kupitia warsha hiyo, wadau wameanza kuandaa mfumo wa kimkakati wa kuhakikisha utambuzi wa ujuzi unaendana na mahitaji ya soko la ajira na kwamba kanuni za ajira zenye staha zinaingizwa rasmi katika sekta ya ubunifu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button