Steve Nyerere: Acheni siasa zisizo na tija

DAR ES SALAAM. MCHEKESHAJI mkongwe na Mwenyekiti wa taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, amewataka Watanzania hususanI vijana kuacha kujikita kupita kiasi kwenye siasa zisizoleta matokeo, badala yake kuelekeza nguvu kwenye shughuli za maendeleo.
Akizungumzia mwenendo wa jamii kwa sasa, Nyerere amesema kumekuwa na hali ya watu wengi kupoteza mwelekeo wa kufanya kazi kwa bidii na kujikuta wakitumia muda mwingi kwenye mambo yasiyo na tija, jambo linalokwamisha maendeleo ya taifa.
Amesema vijana wengi wamekuwa wakivutiwa zaidi na siasa, ubashiri wa michezo (kubeti) pamoja na mitindo mingine isiyowajengea msingi imara wa maisha, hali inayosababisha hata wasomi kushindwa kutumia elimu yao ipasavyo.
“Lazima tuwe na taifa la watu wanaoipa kipaumbele maendeleo. Hatuwezi kusonga mbele kama kila siku ni siasa tu, asubuhi siasa, jioni siasa,” amesema Steve
Aidha, amewahimiza Watanzania kuondokana na hofu inayowazuia kuthubutu kufanya mambo makubwa, akieleza kuwa hofu ni kikwazo kikubwa cha mafanikio kwa wengi.
Katika wito wake, Nyerere amesisitiza umuhimu wa kuona matokeo chanya ya siasa kupitia maendeleo ya taifa, badala ya kubaki kwenye mijadala isiyo na tija.
Pia amegusia matumizi ya mitandao ya kijamii, akitaka itumike kama chombo cha kukuza uchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa, badala ya kutumika kwa malumbano, kudhalilishana na kuchongeana.
Kwa upande mwingine, amewakumbusha Watanzania kujivunia utaifa wao na kuenzi umoja, akieleza kuwa mshikamano na upendo ni nguzo muhimu katika kulisukuma taifa mbele.
Amesema ni wakati wa kila mmoja kusimama kwenye nafasi yake na kuchangia maendeleo ya nchi, huku akihimiza kurejea katika misingi ya maadili, hofu ya Mungu na uwajibikaji.




