Stones karibu kutua Inter Milan

MILAN: Beki wa kimataifa wa England, John Stones, yuko hatua za mwisho kujiunga na mabingwa wa Italia, Inter Milan, baada ya kufikia makubaliano ya awali ya kujiunga na klabu hiyo kwa uhamisho wa bure kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na Manchester City.
Taarifa kutoka Italia zinaeleza kuwa Inter imefanikiwa kuwashinda Arsenal, Chelsea na Juventus katika mbio za kuwania saini ya beki huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili baada ya kukamilisha vipimo vya afya.
Stones anaondoka Manchester City baada ya kuitumikia kwa miaka 10, akichangia mafanikio makubwa yaliyomshuhudia akitwaa mataji kadhaa ikiwemo Ligi Kuu England, UEFA Champions League na Kombe la Dunia la Klabu.
Kiwango chake bora alichokionesha akiwa na timu ya taifa ya England kwenye Kombe la Dunia 2026 kimeongeza imani ya Inter kuwa anaweza kuimarisha safu ya ulinzi ya klabu hiyo katika harakati za kutetea ubingwa wa Serie A na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Iwapo uhamisho huo utakamilika kama inavyotarajiwa, Stones atakuwa mmoja wa usajili mkubwa wa Inter katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi.




