Kwingineko

Southampton katika skendo ya ujasusi

LONDON: KLABU ya Southampton imeomba kuongezewa muda na EFL ili kukamilisha uchunguzi wa ndani kuhusu tuhuma za ujasusi dhidi ya wapinzani wao Middlesbrough kabla ya mchezo wa marudiano wa mtoano wa kuwania kupanda Ligi Kuu England.

Southampton wanatuhumiwa baada ya mchambuzi mmoja wa timu hiyo kudaiwa kurekodi mazoezi ya Middlesbrough akiwa amejificha kwenye vichaka kabla ya mchezo wa kwanza uliomalizika kwa sare tasa.

Mtendaji Mkuu wa Southampton, Phil Parsons amesema klabu hiyo inashirikiana kikamilifu na EFL huku ikiendelea kufanya tathmini ya ndani ili kupata ukweli wote kabla ya hitimisho lolote kufikiwa.

Hata hivyo, viongozi wa Middlesbrough wanataka Southampton waondolewe kabisa kwenye mtoano endapo watapatikana na hatia, wakisisitiza adhabu hiyo iwe ya kimichezo badala ya faini pekee.

Ripoti zinaeleza kuwa EFL inaweza kutoa adhabu mbalimbali kuanzia faini hadi kuifukuza Southampton kwenye mashindano hayo ya kuwania nafasi ya kupanda Premier League, hatua inayohusishwa na zaidi ya pauni milioni 200 za mapato.

Kocha wa Middlesbrough, Kim Hellberg amesema suala hilo ni la kufuata sheria na taratibu za mchezo, huku akidai timu yake iliathirika kwa sababu Southampton ingeweza kupata taarifa muhimu za mazoezi yao ikiwemo maandalizi ya mikwaju ya penalti.

 

Related Articles

Back to top button