Simba ,Knauf zakubaliana mwaka mmoja

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imeingia mkataba mpya wa udhamini wa mwaka mmoja na kampuni ya vifaa vya ujenzi Knauf, wenye thamani ya Sh milioni 200 ikiwa na lengo la kuendeleza michezo nchini.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema wamekaribisha familia mpya ndani ya klabu hiyo kwa kuingia makubaliano na kampuni hiyo katika kuchangia kwenye timu za klabu hiyo.
“Knauf anajiunga kama mdhamini.Mkataba wenye thamani ya Sh milioni 200 na kadri tutakavyokuwa tunaingia mkataba mpya itakuwa ni nafasi ya kuongeza udhamini wao, Simba tuna furaha kubwa kuwakaribisha kampuni hiyo,” amesema.
Ahmed amesema jukumu lao ni kuyashawishi makampuni mengine kwenda Simba sababu ni chapa kubwa Afrika na kila kampuni inatamani kufanya kazi na klabu hiyo ambayo inashika nafasi ya sita katika orodha ya klabu bora Afrika.
Mkurugezi wa Kanda wa Kampuni hiyo Tanzania,IIse Boshoff amesema ni uwekezaji wa kimkakati kwani Simba ni taasisi kubwa hivyo anaona ushirikiano mkubwa na kuangalia namna wanaweza kusonga mbele.
Naye Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema ushirikiano huo wanaamini watafika, jambo kubwa unaongeza thamani ya uwekezaji ndani ya klabu hiyo.
“Sisi hatuangalii sana thamani ya pesa tunayopata, zaidi ni thamani ya mkataba na ukubwa wake,tumeingia mkataba wa ushirikiano wa moja kwa moja, tuna mashindano ya nje na ndani na mkataba ni kwa timu zetu zote,” amesema Mangungu.