Ligi Kuu

Majanga Simba, Mutale Nje

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Simba, Joshua Mutale atahitajika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja kwa ajili ya kuuguza jeraha lake la nyama za paja.

Joshua alipata jeraha la nyama za paja katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa Agosti 18, dhidi ya Tabora United na kutolewa dakika ya 31 ya mchezo huo uliopigwa uwanja wa KMC , uliopo Mwenge, DSM.

Akizungumza na Spotileo Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kiungo huyo atakuwa nje ya uwanja wa siku saba akiuguza jeraha lake.

Amesema hajapata jeraha kubwa na anatarajia baada ya siku hizo endapo ataendelea vizuri na kuwa fiti, kocha Fadlu (Davids), ataangalia uwezekano wa kumtumia.

“Joshua (Mutale) hayupo kwenye mipango dhidi ya Fountain Gate FC kwenye mechi yetu ya Jumapili, Agosti 25. Amepewa siku saba za kupata matibabu ya jeraha lake, “ amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa baada ya siku hizo kupita, jopo la madaktari wa Simba wataendelea kumchunguza na kuangalia kama yupo fiti asilimia 100 kwa ajili ya kucheza mechi zijazo.

Ameeleza kuwa wana kikosi kipana na kutokuwepo kwa nyota huyo kwenye mechi dhidi ya Fountain Gate FC haitawaathiri kwa sababu ya kuwepo kwa mbadala wake ambaye kocha Fadlu atamtumia.

Simba wanatarajia kushuka dimbani Jumamosi Agosti 25, dhidi ya Fountain Gate FC, uwanja wa KMC , uliopo Mwenge Dar es Salaam

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button