Simba tayari kuvaana na Bravos Do Maquis

LUANDA:KIKOSI cha Simba kesho kitaingia uwanja wa 11 de Novembro kusaka alama tatu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola.
Katika mchezo huo timu zote zinahitaji alama tatu ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kucheza robo fainali ya michuano hiyo.
Kocha wa simba Fadlu Davids amesema anaamini utakuwa mchezo mgumu hasa kutokana na jinsi kundi lao lilivyo, lakini wao wamejiandaa vizuri. Amesema Bravos ni tofauti inapocheza nyumbani hivyo amejipanga kuhakikisha wachezaji wamekamilika katika kila idara.
“Tunaifahamu vizuri Bravos ikicheza nyumbani inacheza kivingine na nje ya nyumbani inacheza kwa na,mna nyingine. Wapo vizuri kwenye kuanzisha mashambulizi baada ya kupora mpira, tunatakiwa kumiliki zaidi mchezo,” amesema Kocha Fadlu.
Kwa niaba ya wachezaji kiungo, Debora Fernandes aliyewahi kucheza nchini Angola kwa miaka miwili amesema utakuwa mchezo mgumu kutokana na Bravos kuhitaji alama tatu ili kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali, lakini malengo yao ni kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
“Utakuwa mchezo mgumu. Natambua Bravos wanacheza nyumbani na wanahitaji pointi tatu, kila mmoja anajua malengo ya Simba ni kuhakikisha tunafanya vizuri. Binafsi nimefurahi kurudi nyumbani, nimecheza Angola kwa miaka miwili, nimewaambia wachezaji wenzangu mambo mbalimbali kuhusu hapa ili wajue mazingira na aina ya mchezo utakaochezwa,” amesema Debora.