Ligi Kuu

Okello, Barker watwaa tuzo za Mei Ligi Kuu

DAR ES SALAAM: KIUNGO mshambuliaji wa Yanga Allan Okello, ameendelea kuthibitisha ubora wake baada ya kutangazwa Mchezaji Bora wa Mwezi Mei wa Ligi Kuu msimu wa 2025/26.

Okello ametwaa tuzo hiyo baada ya kuonesha kiwango cha juu mwezi huo kwa kufunga mabao tisa na kutoa pasi moja ya bao katika dakika 509 za michezo sita aliyoichezea Yanga, akichangia timu hiyo kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi.

Katika mchakato wa tuzo hizo uliofanywa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Okello aliwashinda Clatous Chama wa Simba SC na Feisal Salum wa Azam FC ambao waliingia naye hatua ya mwisho ya kuwania tuzo hiyo.

Kwa upande wa makocha, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ametangazwa Kocha Bora wa Mwezi Mei baada ya kuiongoza timu yake kushinda michezo mitano na kutoka sare mmoja katika mechi sita za ligi.
Barker aliwashinda Florent Ibenge wa Azam FC na Felix Minziro wa Fountain Gate FC, huku mafanikio yake yakiiwezesha Simba kuendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Katika tuzo nyingine, Meneja wa Uwanja wa Airtel Singida, Omar Malule, ametajwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Mei kutokana na usimamizi mzuri wa matukio ya michezo na miundombinu ya uwanja huo.

Wakati huo huo, Kamati ya Tuzo ya TFF imetangaza mabao matatu yatakayowania tuzo ya Bao Bora la Mwezi kupitia kura za mashabiki. Mabao hayo ni la Paul Peter dhidi ya Fountain Gate, la Clatous Chama katika dabi kati ya Simba na Yanga, pamoja na la Christopher Tibandeke katika mchezo wa TRA United dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kwa upande wa Ligi ya NBC Championship, Salum Mlemwa wa Gunners FC ametangazwa Mchezaji Bora wa Mwezi Mei baada ya kufunga mabao manne katika dakika 357 za michezo mitano huku Kocha wa Gunners, Henry Mkanwa, akitwaa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuiongoza timu yake kushinda michezo yote minne iliyocheza na kupanda kutoka nafasi ya 11 hadi ya saba kwenye msimamo wa ligi.

Related Articles

Back to top button