Simba, Mafunzo kuchuana Muungano leo Zanzibar

ZANZIBAR: WEKUNDU wa Msimbazi Simba na Mafunzo wanatarajiwa kushuka dimbani leo kuwania ushindi katika michuano ya Kombe la Muungano, utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo ambao tayari umevuta hisia za mashabiki wengi wa soka, unatarajiwa kuanza saa 2:15 usiku.
Wakizungumzia mchezo huo makocha wa timu hizo wamesema amejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo.
Kocha wa Simba, Stevene Barker, amesema wamewasili Zanzibar wakiwa na malengo matatu makuu, likiwemo kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Amesema kuwa lengo lingine ni kutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawapati muda wa kucheza mara kwa mara katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine huku lengo la tatu ni kuijenga upya timu kisaikolojia kabla ya kurejea kwenye ratiba ngumu ya ligi.
Kocha wa Mafunzo, Haji Ramadhan Mwambe, amesema licha ya Simba kuwa timu kubwa, kikosi chake kipo tayari kupambana na kuibuka na ushindi.
Ameongeza kuwa Mafunzo ina mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na vijana chipukizi walio tayari kuonesha uwezo wao dhidi ya wapinzani wao.




