Shamsa Ford: “Naomba talaka zote

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu za Bongo, Shamsa Ford, amefunguka hadharani kuhusu ndoa yake na kumuomba mume wake kumpa talaka zote, akisisitiza kuwa hana nia ya kurejea kwenye uhusiano huo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Shamsa alichapisha video inayomuonyesha akilia huku akieleza kwa hisia kuwa anataka kupewa talaka kamili na si talaka moja, akidai kuwa amefikia uamuzi wa kuhitimisha ndoa yao.
“Naomba talaka zote, sitaki talaka moja. Kwa nini unaning’ang’ania? Umenizaa wewe?” amesema Shamsa, akimaanisha kuwa anahitaji talaka tatu ili kumaliza rasmi ndoa yao kwa mujibu wa imani ya Kiislamu.
Katika ujumbe wake, Shamsa pia alimjibu mume wake ambaye alimtaka aache kuzungumzia masuala yao kwenye mitandao ya kijamii.
“Unaniambia nisilete mambo haya mtandaoni, lakini yalianzia huku. Nilipokupenda kila mtu alijua, na yataishia huku. Mimi sinaga kupepesa,” amesema.
Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku wengi wakisubiri kuona kama mume wake atajibu hadharani kuhusu madai hayo.


