Kwingineko

Ruto aialika Arsenal kutembelea Kenya

NAIROBI, Kenya: RAIS wa Kenya na shabiki mkubwa wa timu ya soka ya Arsenal , William Ruto, ameialika klabu hiyo kutembelea nchini Kenya mwakani kufuatia ushindi wake wa kihistoria wa ubingwa wa Ligi Kuu England uliomaliza ukame wa miaka 22 bila taji hilo.

Ruto alitoa kauli hiyo Juni 18 katika mahojiano maalumu, akieleza kushangazwa na ukubwa wa sherehe zilizotawala jijini Nairobi na maeneo mbalimbali nchini baada ya Arsenal kutangazwa mabingwa wa England. Rais huyo alisema ziara ya klabu hiyo nchini Kenya itakuwa tukio muhimu kwa mashabiki wake wengi waliopo nchini humo.

Akiwa mmoja wa mashabiki wakubwa wa Arsenal, Ruto alifichua kuwa tayari ametuma mwaliko rasmi kwa viongozi wa klabu hiyo na ana matumaini kuwa timu hiyo ya London Kaskazini itakubali kuitembelea Kenya katika kipindi cha mwaka ujao.

“Arsenal hatimaye imefanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kusubiri kwa muda mrefu, na kulikuwa na sherehe kubwa sana. Nilishangazwa na namna wananchi wa Nairobi walivyosherehekea. Nimeanza mchakato wa kuona kama mwaka ujao Arsenal itakuja Kenya,” alisema Ruto.

Rais hiyo aliongeza kuwa ujio wa Arsenal nchini humo utakuwa fursa adhimu kwa mashabiki wake kukutana na wachezaji na viongozi wa klabu hiyo ambayo imejijengea umaarufu mkubwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Maelfu ya mashabiki wa Arsenal walifurika mitaani tarehe 24 Mei baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mbele ya wapinzani wao wakubwa, Manchester City wakiwa wamevalia jezi nyekundu na nyeupe, mashabiki hao waliimba nyimbo za klabu na kupeperusha bendera katika shamrashamra zilizogeuza sehemu kubwa ya mji mkuu wa Kenya kuwa bahari ya rangi za Arsenal.

Sherehe hizo zilisababisha msongamano mkubwa wa magari katikati ya Nairobi huku mashabiki kutoka maeneo mbalimbali nchini wakikusanyika kusherehekea mafanikio ya timu hiyo baada ya kusubiri kwa zaidi ya miongo miwili.

Baada ya ushindi huo, Rais Ruto alijiunga na mashabiki wengi kusherehekea mafanikio ya Arsenal, huku viongozi wengine wa serikali na watu maarufu nchini humo wakituma salamu za pongezi kwa klabu hiyo kwa kuvunja ukame wa muda mrefu wa kutwaa taji la ligi.

Kupitia ujumbe aliouchapisha mtandaoni, Ruto aliisifu Arsenal kwa kuonyesha uthabiti, nidhamu na uvumilivu katika msimu mzima wa mashindano. Alisema mafanikio hayo ni ushahidi kuwa ndoto zinaweza kuchelewa kutimia lakini haziwezi kufutika kabisa ikiwa juhudi na imani vitaendelea kuwepo.

Iwapo mwaliko huo utakubaliwa, ziara ya Arsenal nchini Kenya itakuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo kuwahi kufanyika nchini humo, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona kama mabingwa hao wa England watafika kuungana nao katika kusherehekea mafanikio yao ya kihistoria.

Related Articles

Back to top button