Serikali kuipatia ZIFF eneo la kudumu

ZANZIBAR:SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongeza mwendelezo wa matamasha makubwa ya sanaa yanayofanyika visiwani humo, ikieleza kuwa yamekuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya utalii kwa kuvutia maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi na hivyo kuongeza mchango wa utalii katika uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa msimu wa 29 wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF 2026) katika Ukumbi wa Wangazija wa Wakfu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma, amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa tamasha hilo katika kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia sanaa, utamaduni na utalii.
Amesema kutokana na mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia ZIFF, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika hatua za kuipatia tamasha hilo eneo la kudumu litakalowezesha shughuli zake kufanyika kwa ufanisi zaidi na kuimarisha hadhi yake kama moja ya matamasha makubwa barani Afrika.
Waziri Hamza alisema katika mwaka wa fedha unaoishia mwaka huu Zanzibar imeendelea kushuhudia ongezeko la watalii wanaotembelea visiwa hivyo, huku matukio ya kimataifa ya sanaa na utamaduni yakitajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia mafanikio hayo.
Alieleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na waandaaji wa ZIFF pamoja na wadau wengine wa sanaa ili kuhakikisha tamasha hilo linaendelea kukua na kutoa fursa zaidi za ajira, biashara na maendeleo ya sekta ya ubunifu kwa vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, uongozi wa ZIFF uliishukuru serikali kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa na kueleza kuwa kupatikana kwa eneo la kudumu kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha maandalizi ya tamasha hilo na kuwezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sanaa na filamu mwaka mzima.
Tamasha la ZIFF 2026 limewakutanisha washiriki wa sanaa, filamu na utamaduni kutoka mataifa mbalimbali duniani, huku likitarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa kupitia maonesho ya filamu, majadiliano ya kitaaluma na shughuli mbalimbali za burudani.




