Rayvanny aula Kombe la Dunia 2026 Canada

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kutangaza kuwa atakuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika shughuli za 2026 FIFA World Cup huko Toronto, Canada.
Rayvanny amethibitisha taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo alishiriki ujumbe ulioonesha furaha yake kwa hatua hiyo kubwa katika safari yake ya muziki.
“Ndoto kubwa imekuwa kweli, haya twende Kombe Kombe la Dunia Toronto, tuonane Juni 10, 2026,” ameandika msanii huyo, akionesha jinsi ndoto zake zinavyoendelea kutimia kwenye jukwaa la kimataifa.

Tukio hilo linatajwa kuwa hatua nyingine kubwa kwa nyota huyo wa zamani wa lebo ya WCB Wasafi, ambaye kwa miaka ya karibuni amefanikiwa kujijengea jina nje ya mipaka ya Tanzania kupitia kazi zake zilizovuka Afrika na kupata mashabiki katika mabara mbalimbali.
Kutumbuiza kwenye matukio yanayohusiana na Kombe la Dunia ni heshima kubwa kwa msanii yeyote, kutokana na mashindano hayo kuwa miongoni mwa matukio yanayofuatiliwa zaidi duniani na kukutanisha mamilioni ya mashabiki kutoka nchi mbalimbali.
Rayvanny anaungana na wasanii wengine duniani wakiwemo Nora Fatehi wa India aliyewahi kushirikiana naye, Burna Boy, David Adeleke ‘Davido’, Tyla Laura, Shakira Isabel na wengine kadhaa.
Mwisho




