Rashford hatamsumbua Alisson kesho

LIVERPOOL: MSHAMBULIAJI wa Manchester United Marcus Rashford hajasafiri na kikosi chake na ataukosa mchezo wa Jumapili hii dhidi ya Liverpool dimbani Anfield kutokana na kile kocha wake Ruben Amorim alichotaja kuwa ni mgonjwa.
Rashford alianza kuwekwa kando kwenye mchezo wa dabi dhidi ya jirani zao Manchester City, mchezo ambao United walishinda mabao 2 kwa 1, kisha kukaa nje kwa michezo minne kabla ya kuwekwa benchi katika kipigo chao cha 2-0 kutoka kwa Newcastle Jumatatu. Hata hivyo mshambuliaji huyo hakucheza hata dakika moja.
“Ni hali ya kawaida hiyo, kwa sasa (Rashford) ni mgonjwa. Hafanyi mazoezi. Tutaangalia katika siku zijazo lakini huyu ni mchezaji kama mchezaji mwingine, na mimi ndiye ninaamua nani acheze. Na Marcus ni mgonjwa, Nadhani hatopatikana, wiki hii hatacheza”. Amorim aliwaambia waandishi wa habari kuelekea mchezo huo.
Wakiwa na vipigo vitano katika mechi sita zilizopita za ligi kuu ya England, United wanabarizi katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wakiwa na pointi 22 katika mechi 19. Hii ni nafasi mbaya zaidi kumalizia mwaka tangu wamalize mwaka katika nafasi ya 15 mwaka 1989.