EPL

Pochettino aumizwa na mateso ya Spurs

afunguka hatma ya kurejea

LONDON:KOCHA wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, amesema anahuzunishwa kuona timu hiyo ikipitia kipindi kigumu huku ikipambana kujinusuru kushuka daraja kutoka Premier League.

Pochettino, aliyeinoa Spurs kati ya mwaka 2014 hadi 2019 na kuifikisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, amesema bado ana mapenzi makubwa na klabu hiyo na anaguswa na hali wanayopitia kwa sasa.

“Ninaipenda sana Tottenham. Itabaki kuwa sehemu muhimu ya maisha yangu, si tu kama kocha bali hata binafsi. Inasikitisha kwa sababu najua watu wanavyoteseka ndani ya klabu na hata mashabiki,” amesema Pochettino.

Kwa sasa Tottenham ipo nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa pointi mbili nyuma ya eneo salama huku ikiwa imebakiwa na michezo minne tu kumaliza msimu.

Kocha huyo ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya taifa ya Marekani, pia aligusia uwezekano wa kurejea tena Ligi Kuu England siku zijazo.

“Siku moja inawezekana, kwa sababu napenda sana England. Nafikiri wasifu wangu kama mtu na kama kocha unaendana vizuri na Premier League,” amesema.

Wakati huo huo, hali ya Spurs imezidi kuwa ngumu kutokana na majeraha ya wachezaji muhimu, akiwemo kiungo Xavi Simons na mshambuliaji Dominic Solanke, jambo linalozidi kupunguza matumaini yao ya kubaki ligi kuu.

Related Articles

Back to top button