Pamba yamla kichwa Kapunovic

UONGOZI wa Pamba Jiji umetangaza kuachana na Kocha Mkuu Goran Kapunovic baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba na sasa Mathias Wandida atachukua nafasi yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Ezekiel Ntibikeha Leo, pia, wamefikia makubaliano ya kusitisha mikataba ya wasaidizi wake Salvatory Edward, kocha wa magolikipa Razack Siwa na kocha wa viungo Cirus Kakooza.
Ntibikeha amesema kwa sasa timu itakuwa chini ya Kocha Mathias Wandiba aliyekuwa kocha wao wa timu ya vijana chini ya miaka 20 hadi hapo atakapotangazwa Kocha Mkuu.
“Uongozi unawashukuru kwa muda wao wote waliokuwepo hapo klabuni na unawatakia kila la heri katika maisha yao ya nje ya Pamba Jiji,”amesema.
Tangu kuanza kwa msimu huu Kapunovic hajashinda mchezo hata mmoja katika saba waliyocheza, wakiambulia sare nne na kupoteza michezo mitatu huku timu hiyo ikishika mkia kwa pointi nne.