Mavazi

Masaki: Amani inachochea mafanikio sekta ya mitindo

MBUNIFU wa mavazi kutoka AMFashion, Agusta Masaki, amesema amani iliyopo nchini Tanzania ni nguzo muhimu inayowezesha wabunifu na wafanyabiashara kufanya kazi zao kwa utulivu na ubunifu mkubwa.

Akizungumza na SpotiLEO kuhusu mtazamo wake, Masaki ameeleza kuwa tofauti na baadhi ya nchi nyingine, Tanzania inatoa mazingira rafiki yanayoruhusu watu kufikiria, kuunda na kukuza vipaji vyao bila hofu yoyote.

“Kwa upande wangu kama mbunifu wa mitindo, ninaona amani imenisaidia kukuza kazi yangu kwa kiwango kikubwa. Nimeweza kushirikiana na watu mbalimbali, kushona na kuuza bidhaa zangu kwa uhuru, na hata kufikia masoko mapana zaidi, Kimataifa” amesema Agusta.

Ameongeza kuwa amani inatoa nafasi kwa Watanzania kuota ndoto kubwa na kuzitimiza, hasa kwa vijana wanaojihusisha na sekta ya ubunifu na biashara ndogondogo.

Aidha, Agusta ametoa wito kwa jamii kujikita katika kufanya kazi kwa bidii na kuongeza kipato kupitia mbinu mbalimbali.

Amesisitiza umuhimu wa kujituma na kuwa na nidhamu kazini, kujifunza mitindo mipya ili kuboresha ubunifu, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kama chombo cha kutangaza kazi na kupanua masoko.

Pia amehimiza ushirikiano miongoni mwa wabunifu ili kujenga mtandao imara wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuthamini wateja kwa kutoa huduma bora na yenye kuridhisha.

Agusta amekumbusha kuwa amani si jambo la kawaida, bali ni rasilimali muhimu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania kupitia vitendo vya kudumisha umoja, kuheshimiana na kufanya kazi kwa bidii.

“Kilicho mikononi mwetu kinaweza kuijenga Tanzania bora zaidi, kila mmoja kupitia kile anachokifanya,” amesisitiza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button