“Niko tayari kuondoka United” – Rashford

MANCHESTER ENGLAND: Mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford amesema yuko tayari kwa changamoto mpya baada ya hivi karibuni kuibuka tetesi za nyota huyo kuachana na mashetani wekundu na kuondoka viunga vya Old Trafford alikodumu kwa takriban miaka 20
Rashford ambaye hakuwa sehemu ya kikosi cha United kilichoibugiza Man City 2-1 wikiendi iliyopita alimueleza mwandishi wa habari za michezo wa jarida la World soccer kuwa hana wasiwasi na yuko tayari kuondoka kwa wema ikiwa hahitajiki tena na United.
“Binafsi nadhani niko tayari kwa changamoto mpya, na ikiwa nitaondoka haitakuwa vita, hamtasikia ubaya wa Manchester United kutoka kwangu. Kama najua hali ni mbaya, sitaizidisha kwa kuongea. Nimeona namna wachezaji wengine wanavyoondoka na mimi sitaki kuwa wao nikiondoka taarifa nitatoa mimi” amesema Rashford.
Rashford amefunga mabao matatu tangu kocha mpya Ruben Amorim atwae mikoba ya kuinoa timu hiyo, na hivi karibuni alizomewa na mashabiki wa timu hiyo alipofanyiwa mabadiliko mapema katika kipindi cha pili cha ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Viktoria Plzen kwenye Europa league