Burudani

Zuchu ajizawadia Bentley, Khadija Kopa, Sandra kalibariki

DAR ES SALAAM:MSANII wa Bongo Fleva, Zuhura Othumani maarufu kama Zuchu, amejizawadia gari aina ya Bentley, akielezea kuwa ni sehemu ya matunda ya juhudi, bidii na mafanikio aliyoyapata kupitia kazi yake ya muziki.

Katika tukio hilo la furaha, Zuchu ameamua kumchukua mama yake mzazi pamoja na Sandra, ambapo wote watatu walipanda ndani ya gari hilo jipya.

Msanii huyo anaamini kuwa kuanza safari ya gari hilo akiwa na watu wake wa karibu, hususan mama yake, ni namna ya kuliombea na kulibariki gari hilo.

Akizungumza katika tukio hilo, Zuchu amesisitiza umuhimu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kufanya kazi kwa bidii na kuthamini watu wanaomzunguka pamoja na mashabiki ambao wamekuwa sehemu kubwa ya mafanikio yake.

Zuchu amesema:

“Mwenyezi Mungu, juhudi na sapoti ya watu wanaokuzunguka haijawahi kumuangusha mtu.”

Kwa upande wake, mwanamuziki mkongwe Khadija Kopa alimkumbusha Zuchu kutowasahau mashabiki wake, akieleza kuwa wamekuwa na mchango mkubwa katika safari yake ya mafanikio.

Khadija Kopa pia aliongoza dua maalumu kwa ajili ya gari hilo, huku akimpongeza Zuchu kwa mafanikio aliyoyapata kupitia muziki.

Katika salamu zake za pongezi, Khadija Kopa alisema:

“Usingekuwa msanii, sasa hivi ungekuwa kwangu unasugua masufuria. Usingepata gari kama hii. Sifa zote wapewe Wasafi.”

Tukio hilo limekuwa sehemu ya furaha na shukrani kwa Zuchu, huku likionyesha pia nafasi ya familia, mashabiki na watu waliomzunguka katika safari yake ya mafanikio ya muziki.

Related Articles

Back to top button