Mastaa

Ammy Gal:“Sikuwa na sehemu ya kuita nyumbani”

DAR ES SALAAM:MREMBO na tangazaji wa kipindi cha The Switch, Ammy Gal, amewagusa wengi baada ya kufunguka kuhusu changamoto za maisha alizopitia, akieleza kuwa kwa sasa anajitahidi kujenga makazi yake ili apate sehemu atakayoweza kuiita nyumbani.

Kupitia kauli yake, Ammy Gal amesema amekuwa akiishi bila kuwa na sehemu maalumu ambayo anaweza kuitambua kama nyumbani kwake, tofauti na watu wengine wenye familia na makazi wanayoweza kuyategemea wanapokumbwa na changamoto.

Ameeleza kuwa hata anapopatwa na tatizo la ghafla au kuanguka, hana sehemu maalumu ambayo anaweza kupelekwa na kujihisi yupo nyumbani. Hali hiyo imemfanya kuongeza juhudi katika kujitengenezea maisha na makazi yake mwenyewe.

Aidha, mtangazaji huyo ametoa ujumbe kwa watu wenye familia na sehemu za kuziita nyumbani, akiwataka kuzithamini, kuziheshimu na kuzipenda, akiwakumbusha kuwa wapo watu wengi ambao hawana hata sehemu ya kusema, “Hapa ni nyumbani kwangu.”

Ammy Gal pia amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mafanikio ya wengine na kuacha tabia ya kuwavunja moyo, akieleza kuwa si kila mtu anayepambana na maisha huweka wazi maumivu na changamoto anazopitia nyuma ya pazia.

Kauli yake imeibua tafakari kuhusu maisha, familia na umuhimu wa kuthamini kile tulichonacho, huku ikitoa ujumbe kuwa mafanikio ya mtu hayapaswi kuhukumiwa kwa mwonekano wa nje pekee.

Ujumbe wa Ammy Gal ni ukumbusho kwamba kuwa na familia na sehemu ya kuiita nyumbani ni jambo la thamani kubwa ambalo si kila mtu amebahatika kuwa nalo.

Related Articles

Back to top button