Kikapu

Dar City yapata nafasi ya 16 bora BAL

DAR ES SALAAM: MABINGWA wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam, Dar City wamepata nafasi ya moja kwa moja kushiriki hatua ya 16 bora ya mashindano ya kuwania nafasi za Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika (BAL), bila kupitia hatua ya makundi ya awali.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani (FIBA), Dar City ni miongoni mwa timu tatu zilizopewa nafasi hiyo moja kwa moja, nyingine zikiwa Nairobi City Thunder ya Kenya na Jeunesse Club d’Abidjan Kings ya Ivory Coast.

Wakati Dar City na timu hizo mbili zikipata nafasi ya moja kwa moja, timu nyingine nane kutoka ukanda wa Mashariki zimefanikiwa kufuzu hatua hiyo baada ya kukamilika kwa michezo ya makundi.

Timu hizo ni Nairobi City Thunder ya Kenya, Urunani BC ya Burundi, NAM Blazers ya Uganda, Ferroviario ya Msumbiji, Munali Suns ya Zambia, Dolphins BC ya Botswana na Patriots BC ya Sudan Kusini, huku Dar City ikiwa mwakilishi mwingine kutoka Tanzania.

Hatua ya 16 bora kwa timu za ukanda wa Mashariki inatarajiwa kufanyika jijini Nairobi, Kenya, kuanzia Novemba 24 hadi 29, mwaka huu, ambapo timu zitachuana kuwania nafasi ya kufuzu fainali za mashindano hayo.

Katika hatua hiyo, timu zitagawanywa katika makundi mawili yenye timu nne kila moja, huku zikisaka nafasi ya kuendelea na safari ya kuwania ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Afrika wa mwaka 2027.

Related Articles

Back to top button