Neo Maema akoshwa na umoja Simba

DODOMA: UMOJA na morali kubwa ndani ya kikosi cha Simba ndivyo vinavyompa furaha zaidi kiungo Neo Maema, akiamini kuwa mshikamano wa timu hiyo ndiyo silaha muhimu katika safari ya kusaka ubingwa msimu huu.
Maema amesema pamoja na kufurahia mwenendo mzuri wa timu, anaona kitu cha pekee ni namna wachezaji wanavyokuwa kitu kimoja ndani na nje ya uwanja.
Amesema kuwa wachezaji wachache wanaweza kuamua matokeo ya mechi, lakini timu yenye umoja ndiyo inayoweza kubeba mataji mwishoni mwa msimu.
“Furaha iliyopo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na namna wachezaji wanavyoshikamana ndiyo jambo kubwa kwangu, kwa sababu najua inahitajika nini ili kushinda ligi. Ni safari ndefu, hivyo ni muhimu kuendelea kuwa pamoja,” amesema Maema.
Kiungo huyo amesema wataendelea kujipanga vizuri kwa kila mchezo kutimiza majukumu yao ya kusaidia timu kufikisha malengo iliyojiwekea.




