Mastaa

Mawakili wa Diddy waomba kujitoa kesi

....wadai hawajalipwa

NEW YORK: MAWAKILI wanaomwakilisha msanii wa Marekani, Sean ‘Diddy’ Combs, katika kesi za madai wameiomba mahakama ya shirikisho kuwaruhusu kujitoa kwenye uwakilishi, wakidai kuwa msanii huyo hajawalipa ada za uwakili kwa zaidi ya miezi sita.

Mmoja wa mawakili hao, Michael Tremonte wa kampuni ya Sher Tremonte LLP, amesema kampuni hiyo bado inamdai Combs kiasi kikubwa cha fedha kutokana na huduma za kisheria ilizompatia.

Tremonte pia amedai kuwa kampuni hiyo haijafanikiwa kufanya mawasiliano ya maana na Combs kwa zaidi ya miezi minne kuhusu kesi zinazomhusu.

Mawakili hao walikuwa wakimwakilisha Combs katika kesi ya madai ya fidia ya dola milioni 100 iliyowasilishwa na msanii huyo dhidi ya Courtney Burgess, wakili Ariel Mitchell na Nexstar Media, kampuni inayoendesha kituo cha televisheni cha NewsNation.

Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa mahakamani, mawakili hao wameomba ruhusa ya kujiondoa katika kesi hiyo kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano na kutolipwa ada zao kwa kipindi walichokitaja.

Hata hivyo, Combs amepinga madai hayo kupitia msemaji wake, akisema uamuzi wa kubadili timu yake ya mawakili umetokana na kile alichodai kuwa ni kutozwa gharama ambazo hakuwahi kuziidhinisha.

Msemaji huyo amesisitiza kuwa suala hilo ni mgogoro wa kibiashara unaohusu ada za uwakili, huku Tremonte akikanusha madai kwamba kampuni yake ilimtoza Combs zaidi ya kiwango kilichostahili.

Hatua hiyo imeongeza mvutano mwingine wa kisheria unaomkabili Combs, wakati kesi mbalimbali zinazohusisha jina lake zikiendelea kushughulikiwa mahakamani.

Related Articles

Back to top button