Al-Taawoun yatozwa milioni 71.4 na kucheza bila mashabiki

RIYADH: Klabu ya Al-Taawoun imepewa adhabu na Shirikisho la Soka la Saudi Arabia baada ya baadhi ya mashabiki wake kuhusishwa na kauli za mashabiki zilizomlenga marehemu Diogo Jota wakati wa mchezo dhidi ya Al-Hilal.
Al-Taawoun imeamriwa kucheza michezo miwili ya nyumbani bila mashabiki, huku pia ikitozwa faini ya riyal 100,000 za Saudi Arabia sawa na milioni 71.4 za Tanzania, kufuatia tukio hilo lililotokea katika mchezo wa Saudi Pro League dhidi ya Al-Hilal.
Katika mchezo huo, baadhi ya mashabiki wa Al-Taawoun walitamka jina la Jota wakimlenga kiungo wa Al-Hilal, Rúben Neves, ambaye alikuwa rafiki wa karibu na aliyekuwa mchezaji mwenzake wa Jota katika klabu na timu ya taifa ya Ureno.
Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa baada ya Neves kuonekana akijibu kwa ishara akiwa uwanjani.
Diogo Jota alifariki mwaka 2025 katika ajali ya gari nchini Hispania, pamoja na kaka yake André Silva.
Baada ya tukio hilo, Al-Taawoun, Al-Hilal pamoja na mamlaka za soka nchini Saudi Arabia walilaani mwenendo huo, wakisema kutumia misiba binafsi kuwachokoza au kuwadhihaki wengine hakukubaliki katika soka.
Nyota wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, pia alitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya mashabiki waliohusika, akisema watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo hawapaswi kuruhusiwa kuingia tena viwanjani.
Adhabu hiyo imeongeza mjadala kuhusu nidhamu na mwenendo wa mashabiki katika soka la Saudi Arabia, huku Al-Taawoun ikilazimika kucheza michezo yake miwili ijayo ya nyumbani bila uwepo wa mashabiki.




