Patcho Mwamba awasihi wasanii kujifunza Live band
RAIS wa Bendi ya Fm Academia Patcho Mwamba amewashauri Wasanii wa muziki wa Bongo fleva kujikita zaidi katika kuimba muziki wa mubashara (live) ili kuwapa raha mashabiki kufurahia kazi zao.
Akizungumza na Spoti leo, Patcho Mwamba amesema wasanii wanatakiwa kuujua muziki na kupiga vyombo vya Kimuziki ili wawe wanamuziki na sio kuishia kuwa waimbaji.
“Niwaombe wasanii wa Bongo fleva kutosita kujifunza kutoka kwa wasanii wenzao kama Ali Kiba, ukimtazama akiwa jukwaani unaona kabisa kwamba anajua anachokifanya hadi unafurahia kusikiliza anachokiimba. Wapo wasanii wanaojitahidi kuimba vizuri wawapo jukwaani kama Alikiba, Mbosso pamoja na Jaydee, “amesema Patcho Mwamba.
Amesema kuwa Msanii ukijua kupiga tumba, Solo, Gita na vingine itakusaidia zaidi kutumbuiza kwa aina ya Live band na hata malipo yataongezeka zaidi.
Patcho amesema Wakongo wamekuwa wakifanya vizuri kwa upande wa kupiga muziki wa mubashara (Live band) kutokana na wao kujikita katika kujifunza vyombo mbalimbali vya Kimuziki.