Mwanasheria Yanga ateuliwa ngumi za kulipwa
KAMATI ya mpito ya Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini, TPBRC imemteua Mwenyekiti wa kamati ya mabadaliko na Mwanasheria wa Yanga,Alex Mgongolwa katika kamati ndogo ya kuboresha katiba na kanuni za mchezo huo.
Wengine walioteuliwa kwenye kamati hiyo, Jimmy Kabwe mtaalam masoko ya michezo, bondia wa zamani, Joseph Marwa pamoja na daktari wa tiba ya mwili wa binadam (Physiothelapy), Fredireck Mashahili.
Kaimu Katibu Mkuu, Nsajigwa Mwangamilo amesema kamati hiyo kwa lengo kuboresha katiba na kanuni za mchezo huo ambapo itahusisha wataalamu kutoka katika taasisi tatu za tasnia tofauti.
“Mgongolwa wanasheria wakongwe na wazoefu katika tasnia ya michezo na ameshiriki katika mapinduzi ya tasnia ya michezo ikiwemo mpira wa miguu na Kabwe ni mtaalam wa masoko na Sports Busness kwenye michezo, mdau mkubwa wa mchezo wa ngumi, tunaamini atatusaidia katika eneo la masoko.
Pia yupo bondia wa zamani anajua vizuri mchezo wa ngumi na ameshiriki katika kuandaa katiba mbalimbali za mchezo huu nchini pamoja na Dk Fredirick Mashahili ambaye ni mbobezi wa tiba ya mwili,” amesema Nsajigwa.
Mbali ya hayo,TPBRC imetoa maelekezo kuwa mdau anayehusika na shughuli za ngumi za kulipwa kwenye ulingo atapaswa kuwa na leseni za Kamisheni hiyo kuanzia sasa.
Amesema maelekezo mengine ni muda wa kumaliza mapambano ya ngumi itakuwa saa sita kasoro usiku, mapambano madogo hayatakiwi kizidi bout 15 na makubwa hayatakiwi kuzidi bout 10.
“Tumekuwa tukifanya mabadiliko ya mchezo wa ngumi kwa kuzungumza na mapromota na mabondia tufanye mapinduzi na kupelekea uwe katika njia sahihi,” amesema Kaimu katibu wa mkuu wa TPBRC.