Etihad yatishia kuishitaki Ligi Kuu ya England

MANCHESTER, England: SHIRIKA la ndege la Etihad Airways, ambaye ndiye mdhamini mkuu wa klabu ya Manchester City, limesema linatarajia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Ligi Kuu ya England (Premier League) kufuatia uamuzi wa tume huru iliyobaini ukiukwaji mkubwa wa kanuni za kifedha unaohusishwa na klabu hiyo.
Uamuzi huo umetolewa baada ya tume huru kubaini kuwa Manchester City ilikiuka zaidi ya kanuni 100 za kifedha katika kipindi cha miaka tisa, kuanzia mwaka 2009 hadi 2018, suala lililozua mjadala mkubwa katika soka la England.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tume ilibaini kuwepo kwa mikataba ya kibiashara iliyotajwa kuwa ya udanganyifu, iliyodaiwa kuongeza mapato ya klabu na kupunguza gharama kwa zaidi ya pauni milioni 900, sawa na takribani dola bilioni 1.2.
Etihad, ambayo ni mdhamini mkuu wa jezi za Manchester City na pia ina haki za jina la uwanja wa klabu hiyo, imekataa kuhusishwa na mipango yoyote isiyo halali ya kibiashara. Kampuni hiyo imesema inapingana na hitimisho lolote linaloashiria kuwa ilihusika katika makubaliano yasiyofaa.
Kupitia msemaji wake, Etihad imesema ina wasiwasi kuhusu namna taarifa za uamuzi huo zilivyowasilishwa kwa umma, ikieleza kuwa taarifa zilizovuja na kuripotiwa kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo zimeathiri taswira ya kampuni hiyo, licha ya jina lake kutotajwa katika nyaraka zilizochapishwa.
Kampuni hiyo imesema itatafuta ushauri wa kisheria ili kubaini hatua zinazoweza kuchukuliwa kulinda maslahi yake. Hata hivyo, haijaweka wazi ni hatua gani hasa itachukua au lini inaweza kuanza mchakato huo.
Wakati huo huo, adhabu inayoweza kukabili Manchester City bado haijafahamika, huku kanuni za Ligi ya England zikiruhusu hatua mbalimbali, ikiwemo kupunguziwa pointi, kutozwa faini au kushushwa daraja. Manchester City imeendelea kupinga tuhuma hizo na imesema itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.




