Nyumbani

Kessy: Simba mtakavyokuja, ndivyo tutakavyowapokea

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa JKT Queens, Kessy Juma amesema hawawahofii wapinzani wao Simba Queens kwenye fainali ya Ngao ya Jamii, akisisitiza namna watakavyokuja ndivyo watakavyowapokea.

Kessy ameeleza hayo akifafanua kuwa anakiamini kikosi chake kilivyojipanga na kwamba kesho Jumamosi hawatawaangusha mashabiki wao katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

“Ukichukulia uzani kwamba sisi ni mwabingwa wa Ngao ya Jamii, basi tunakwenda kuitetea na naamini tutapata matokeo mazuri katika mchezo huu.

“Sisi huwa tunampokea mpinzani vile anavyokuja, kwa hiyo nitegemee tu kwamba tutawafurahisha mashabiki wetu, sababu tuna vijana, tuna kikosi kizuri, tumejiandaa vizuri, naamini hatuna sababu ya kukosa matokeo mazuri katika mchezo huu,” alisema Kessy.

Upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ amesema wanaingia uwanjani wakijua wamebakiza hatua moja ili kuanza msimu vizuri kwa malengo waliyojipangia ya kuchukua ubingwa huo walioukosa msimu uliopita.

“Msimu uliopita tulikosa Ngao ya Jamii lakini msimu huu ili tuanze vizuri ilitupasa tushinde mechi ya kwanza twende fainali na tupo fainali ambayo ni faraja kwetu na ndio ukubwa wa Simba. Na sio fainali tu inatakiwa tupambanie kupata kilichopo kwenye hii fainali.

“Lakini pia tunajua mashabiki wanataka furaha, tunafurahi wanatusapoti sana mpaka mikoani, wanafahamu timu inawahitaji na wanakuja viwanjani kupata furaha, na sisi wajibu wetu ni kuwapa furaha kesho, hatutawaangusha,” alisema Mgosi.

Simba ilitinga fainali baada ya kuitungua Yanga Princess kwa mabao 3-0 huku JKT ikiichapa Mashujaa Queens bao 1-0.

Aidha, fainali hiyo itakuwa marudiano ya fainali ya mwaka jana, ambapo JKT iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo, hivyo ni aidha JKT kuendeleza ubabe au Simba kufuta uteja na kutangaza utawala mpya.

Related Articles

Back to top button