Kikapu

NBA yafunga shule ya vipaji afrika kuhamia Abu Dhabi

DAKAR, Senegal: LIGI ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) imefunga akademi yake pekee ya mafunzo ya kiwango cha juu barani Afrika, iliyokuwa nchini Senegal, hatua inayozua wasiwasi kuhusu fursa za vijana wa Afrika wanaotamani kucheza ligi za kulipwa.

Akademi hiyo inayojulikana kama NBA Academy Africa ilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wa Afrika kupitia mafunzo ya kitaalamu, elimu na maandalizi ya kujiunga na timu kubwa za mpira wa kikapu duniani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Reuters iliyochapishwa Oktoba 1, 2026, akademi hiyo imewahi kutoa mafunzo kwa takribani wanafunzi 110. Baadhi yao wamefanikiwa kujiunga na shule na vyuo vikuu vikubwa nchini Marekani, huku wengine wakipata nafasi ya kucheza katika Ligi ya NBA.

Miongoni mwa wachezaji waliopitia akademi hiyo ni Ulrich Kamka Chomche kutoka Cameroon, aliyechaguliwa katika mchakato wa kuingiza wachezaji wapya NBA mwaka 2024, pamoja na Khaman Maluach kutoka Sudan Kusini, anayeichezea Phoenix Suns.

Baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa akademi hiyo wameeleza kusikitishwa na uamuzi wa kuifunga, wakisema unaweza kupunguza fursa kwa vijana wa Afrika, hasa wale wanaotoka katika mazingira magumu na wanaohitaji msaada maalumu ili kufikia kiwango cha juu cha ushindani.

Hata hivyo, NBA imesema uamuzi huo unatokana na mabadiliko ya mkakati wake wa kuendeleza mpira wa kikapu duniani. Ligi hiyo imeeleza kuwa mafunzo yatahamishiwa katika akademi mpya ya kimataifa inayotarajiwa kufunguliwa Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.

NBA imeongeza kuwa itaendelea kuwekeza katika vipaji vya Afrika kupitia programu nyingine, zikiwemo Basketball Africa League na Basketball Without Borders, ikisisitiza kuwa kufungwa kwa akademi ya Senegal hakumaanishi imepunguza dhamira yake ya kukuza vipaji barani Afrika.

Related Articles

Back to top button