Kwingineko

Zidane: Sijutii kumpiga kichwa Materazzi

SAINT-DENIS, Ufaransa: KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Ufaransa, Zinedine Zidane, amesema hana majuto kuhusu tukio la kumpiga kichwa Marco Materazzi wa Italia katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2006, ingawa amesisitiza kuwa hajivunii kilichotokea.

Zidane ametoa kauli hiyo kuelekea mchezo wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya kati ya Ufaransa na Italia, unaotarajiwa kuchezwa leo katika Uwanja wa Stade de France, ikiwa ni mechi yake ya kwanza ya nyumbani tangu alipoteuliwa kuinoa timu hiyo.

Akizungumzia tukio hilo lililomfanya atolewe nje kwa kadi nyekundu katika dakika za nyongeza za fainali ya mwaka 2006, Zidane amesema picha za tukio hilo zimeendelea kuoneshwa mara kwa mara, lakini anapendelea kukumbuka mambo mazuri aliyoyafanya katika maisha yake ya soka.

Amesema hana majuto kwa sababu tukio hilo ni sehemu ya historia ya maisha yake ya soka, ingawa hajawasiliana na Materazzi tangu usiku wa fainali hiyo iliyochezwa mjini Berlin, Ujerumani, ambapo Italia ilitwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti.

Zidane, mwenye umri wa miaka 54, aliteuliwa kuwa kocha wa Ufaransa mwishoni mwa Julai mwaka huu, akichukua nafasi ya Didier Deschamps aliyeondoka baada ya kuitumikia timu hiyo kwa miaka 14. Katika mechi zake mbili za kwanza, Ufaransa ilishinda mabao 1-0 dhidi ya Uturuki na Ubelgiji.

Kocha huyo amesema kurejea Stade de France kutakuwa na hisia kubwa kwake, akieleza kuwa mara ya mwisho kucheza katika uwanja huo ilikuwa mwaka 2006 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mexico. Mchezo wa leo unatarajiwa kuhudhuriwa na mashabiki takribani 80,000.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Ufaransa Ousmane Dembele amekanusha kuwepo kwa mgogoro kati yake na Kylian Mbappe kuhusu tuzo ya Ballon d’Or. Dembele amesema wawili hao wamezungumza na hakuna tatizo kati yao, akieleza kuwa madai ya kutofautiana yaliyosambaa mitandaoni hayana uzito mkubwa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button