Msondo ngoma kuadhimisha miaka 60

DAR ES SALAAM:TAMASHA la Miaka 60 ya bendi ya Msondo ngoma linatarajiwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu katika viwanja vya Gwambina Lounge zamani TCC Club Changombe, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam meneja wa bendi ya Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, amesema kuwa bendi hiyo itaweka kambi ya wiki mbili mkoani Dodoma kwa nia ya kujifua zaidi.
“Msondo ngoma tuna jambo letu la Miaka 60 kuanzishwa. Tamasha la sasa litakuwa na vitu vizuri na ubunifu na ndani ya miaka 10 iliyopita kuna wanamuziki wengi waliojiunga na bendi.
“Waimbaji wanafanya mazoezi ya kutosha siku hiyo wataimba ‘live’ ili kukonga nyoyo za mashabiki wao wanaoipenda Msondo Ngoma wakati wote wanapotoa burudani”,amesema Kibiriti
Kwa upande wake Msanii Freshi Jumbe anayeishi nchini Japan aliyetamba na wimbo wa ‘penzi ni kikohozi’ amesema kuwa ni miongoni mwa waimbaji wa bendi ya Msondo na ameimba nyimbo nyingi ambazo anazifanyia mazoezi na ataimba siku hiyo.
Tamasha la Miaka 60 ya Msondo litasindikizwa na Twanga Pepeta, Ally Choki, Nyoshi El Sadati Rais wa Milele, Spidoch Band ‘Wazungu weusi’ pamoja na msanii wa Bongo fleva Bernard Paul ‘Ben pol’.