Kwingineko

Mpiganaji Mzimbambwe alalamikia familia yake

Adai walifurahia kupigwa kwake

LAS VEGAS: MPIGANAJI wa UFC wa Zimbabwe, Themba Gorimbo ameeleza masikitiko yake kwa familia yake akidai walisherehekea alivyoshindwa katika pambano lake la UFC 310 lililopigwa Desemba 7, 2024.

Hiki kilikuwa kipigo kichungu cha kwanza kwa Mzimbambwe huyo baada ya kushinda mara nne mfululizo kwenye UFC, ambapo alipata ushindi dhidi ya Takashi Sato, Pete Rodriguez, Ramiz Brahimaj na Niko Price.

Gorimbo alipambana na Luque katika pambano la uzito wa welter mnamo Desemba 7, lakini pambano hilo halikuchukua muda mrefu. Mkongwe huyo alimshinda Mzimbabwe huyo katika muda wa sekunde 52 tu.

Luque aliingia kwenye pambano hilo akiwa mtu wa chini lakini alimshangaza Gorimbo (14-5 MMA, 4-2 UFC) huko Las Vegas na kumaliza haraka.

Hadithi ya nyota huyo wa MMA wa Zimbabwe, Gorimbo ilienea sana mwaka 2023 alipokutana na nyota wa filamu na nyota wa WWE, Dwayne Johnson maarufu ‘The Rock’, ambaye alimzawadia nyumba huko Miami nchini Marekani ikiwa sehemu ya kutimiza ndoto zake.

Gorimbo amesema wanafamilia walisherehekea kupoteza kwake ndani ya sekunde 52. Hata hivyo, alisema alilazimika kukabiliana na jamaa waliokuwa wakisherehekea kushindwa kwake, imemuumiza mno kupokea video fupi ikiwaonesha ndugu zake wakisherehekea kushindwa kwake.

“Baadhi ya binamu zangu walikuwa wakisherehekea kupoteza kwangu. Walinitumia video yao mahali ambapo tulikuwa miaka 15 iliyopita, wakiwa katika mduara mdogo huko Danun, ni sehemu yenye makazi duni huko Zimbambwe. Imeniumiza sana,” Gorimbo ameeleza kwenye The Pivot Podcast kupitia MMA Junkie.

“Ninachofanya ni kujaribu kufanya vizuri zaidi kwa kila mtu. Huenda nisisaidie mtu mmoja, lakini nikijenga kisima kinasaidia jumuiya yote na ndugu zangu wakiwemo ila wao kila wakati wananitumia ujumbe wanataka niwatumie dola 5,000. ‘Nipe $5,000’ nitapata wapi hiyo? Watu wanafikiri kwamba mimi niko katika UFC, na mimi ni milionea. Mimi si milionea labda siku moja nitakuwa, ila kwa sasa siwezi kumsaidia pesa kila mtu,” Ameeleza Gorimbo.

 

Related Articles

Back to top button