Kwingineko

Messi hapoi Marekani

LIONEL Messi amefunga magoli mawili na kutoa pasi moja ya bao katika mechi yake ya kwanza kuanza kwenye mchezo akiwa Inter Miami huku timu hiyo ikishinda 4-0 katika mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Atlanta United.

Nyota huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 36 amefunga magoli hayo dakika 22 za kipindi cha kwanza kabla ya kutoa pasi iliyozaa goli la Robert Taylor katika kipindi cha pili.

Baada ya kufunga goli la pili Messi alishangailia kwa kuelekeza kwa mmiliki wa Inter Miami, David Beckham.

“Anaweza kufanya kila kitu kwenye mpira. Anaweza kuumiliki katika nafasi ngumu, na hufanya uamuzi sahihi asilimia 100 ya wakati. Ni ndoto kutimia kucheza naye,”amesema Robert Taylor.

Siku tatu zilizopita Messi alifunga goli la ushindi la Inter Miami wa magoli 2-1 dhidi ya Cruz Azul akitokea benchi katika mchezo wake wa kwanza tangu kuhamia Marekani katika mchezo uliotazamwa zaidi katika historia ya soka Marekani.

Messi, ambaye ni mshindi mara saba wa tuzo ya mchezaji bora duniani ‘Ballon d’Or’, ameanza mazoezi na wachezaji wenzake kwa mara ya kwanza wiki iliyopita tu baada ya kuhamia Ligi Kuu Marekani(MLS) kufuatia mkataba wake Paris Saint-Germain kumalizika.

Ushindi huo wa Inter Miami dhidi ya Atlanta United umeifikisha hatua ya mtoani ya Kombe la Ligi.

Related Articles

Back to top button