Mkakati kwa wageni wa Afcon 2027 wawasilishwa

DAR ES SALAAM:MWENYEKITI wa Kamati Tendaji ya Huduma kwa Wageni wa AFCON 2027, Danford Emmanuel, amewasilisha rasmi Mkakati wa Taifa wa utoaji wa huduma kwa wageni watakaowasili nchini kushiriki na kuhudhuria mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Wasilisho hilo limefanyika Juni 16, 2026, katika ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yanayoendelea kuhakikisha Tanzania iko tayari kupokea maelfu ya wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na duniani.

Mkakati huo unalenga kuboresha huduma kwa wageni kuanzia mapokezi, usafiri, malazi, utoaji wa taarifa, usalama, pamoja na uratibu wa huduma mbalimbali, ili kuhakikisha washiriki na mashabiki wanapata huduma zenye viwango vya kimataifa.
Kikao hicho kimewakutanisha wajumbe wa Kamati Tendaji ya Huduma kwa Wageni wa AFCON 2027, ambao walijadili na kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa mkakati huo kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inaandaa mashindano yenye mafanikio na kuacha taswira nzuri kwa wageni watakaotembelea nchi wakati wa AFCON 2027.




