Africa

Rais Samia azibeba Simba, Yanga 2022/23

MSIMU wa 2022/23 umekuwa na neema kwa nchi ya Tanzania, ambayo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya soka imeenda kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga imekuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika tangu mfumo ulipobadilishwa mwaka 2004 na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Kombe la Shirikisho lilipatikana baada ya kuyaunganisha Kombe la Caf na Kombe la Washindi, hivyo kupata mashindano mapya ambayo yalianza rasmi mwaka 2004 na bingwa wa kwanza akiwa Hearts of Oak ya Ghana.

Hadi sasa ni klabu ya CS Sfaxien ya Tunisia ndio inaongoza kutwaa taji hili ikishinda mara tatu mwaka 2007, 2008 na 2013 timu inayofuata ni Raja Casablanca, TP Mazembe, RS Berkane na Etoile du Sahel, ambazo kila moja imetwaa mara mbili.

Bingwa mtetezi wa mashindano haya alikuwa RS Berkane, ambaye aliondolewa kwenye hatua ya mtoano na US Monastir hivyo kombe halina mwenyewe.

Wakati Yanga ikiwa fainali kwenye Shirikisho timu ya Simba yenyewe iliishia hatua ya robo fainali katika Klabu Bingwa Afrika baada ya kuondolewa na mabingwa watetezi wa taji hilo, Wydad kwa penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1.

Hivyo kama taifa macho yote yamebaki kwa Yanga ambao hadi sasa wamekuwa gumzo barani Afrika kwa kushinda kwenye viwanja vigumu barani Afrika.

Nyuma ya mafanikio haya amesimama Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameirudisha Tanzania kwenye medani ya soka baada ya kupotea kwa muda mrefu huku timu zikishiriki na kuishia hatua za chini.

Awamu ya sita imekuwa na upekee zaidi, mosi kwa kuufanya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuchezwa fainali ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2007.

Hii imetokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia, ambaye licha ya kutingwa na shughuli nyingi lakini amekuwa akitenga muda wake kwa ajili ya kuzisapoti timu zetu kubwa ambazo zimekuwa nembo ya taifa hili.

Rais Samia amekuwa akitoa motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa kununua mabao yanayofungwa na timu hizi kuanzia hatua ya makundi hadi hapa Yanga ilipofika.

Alianza kwa kununua bao moja Sh milioni tano kwenye hatua ya makundi na robo fainali huku nusu fainali ikifika milioni 10 na fainali ikiwa milioni 20 kwa kila bao litakalofungwa.

Hadi sasa jumla ya mabao 26 yamefungwa na Rais Samia ameyalipia, hii yote ikiwa ni motisha ili kuhakikisha Tanzania inaleta taji. Yanga imefunga jumla ya mabao 15 ikifunga mabao tisa kwenye hatua ya makundi, mawili robo fainali na manne kwenye hatua ya nusu fainali.

Simba hadi inaondolewa hatua ya robo fainali ilikuwa imepachika mabao 11 ikifunga mabao 10 kwenye hatua ya makundi na bao moja hatua ya robo fainali.

Rais Samia pia kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ametoa jumla ya tiketi 5,000 kwa ajili ya mashabiki ambao wanatakiwa kwenda kuiunga mkono kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Lakini pia ametoa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 260 itakayoenda na timu pamoja na mashabiki nchini Algeria kwenye mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho barani Afrika ili kuepusha adha ya usafiri baada ya mchezo kukamilika.

YANGA YAVUNA FEDHA

Wawakilishi hawa pekee wa Tanzania na kanda ya Cecafa ndio vinara waliovuna fedha nyingi za Rais Samia, ambapo hadi hatua ya nusu fainali imechota kiasi cha Sh milioni 95 kwenye mabao 15 waliyofunga.

Ilikusanya Sh milioni 45 kwenye hatua ya makundi, milioni 10 kwenye hatua ya robo fainali huku nusu fainali ikijitwalia milioni 40.  Kiasi hiki kimewapa motisha wachezaji ambao wameamua kupambana ili kutomuangusha Rais Samia ambaye hadi sasa tayari rekodi yake imeendelea kuwa nzuri.

Yanga bado wana nafasi ya kuvuna zaidi fedha za Rais Samia kwani wamebakiwa na michezo miwili ya fainali wa kwanza utakaochezwa Benjamin Mkapa kesho Mei 28 na ule wa marejeano utakaochezwa Juni 3 kwenye dimba la Omar Hamadi Stadium nchini Algeria.

Na katika kila bao watakalofunga Yanga katika mchezo watakaoshinda, Samia ameahidi Sh milioni 20, hivyo timu hiyo bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kuvuna fedha za motisha za Mama.

Hii itakuwa mara yao ya pili kucheza kwenye uwanja huo kwani mwaka 2018 ilipoteza kwa mabao 4-0 hivyo inaenda kutafuta nafasi ya kulipa kisasi.

SIMBA ILICHOVUNA

Wekundu wa Msimbazi wao safari yao iliishia hatua ya robo fainali ambako ilikuwa imefunga mabao 11 kati ya hayo 10 yalifungwa kwenye hatua ya makundi na moja likifungwa kwenye mchezo wa robo fainali.

Hadi inaondolewa na Wydad, Simba imejikusanyia jumla ya Sh milioni 55, ambazo ilikuwa kama motisha ambapo hatua ya makundi ilichukua kiasi cha Sh milioni 50 na robo fainali ikijinyakulia milioni tano.

Related Articles

Back to top button