Messi azua hofu Kombe la Dunia 2026

MIAMI: Nyota wa timu ya taifa ya Argentina , Lionel Messi, amezua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kupata maumivu wakati akiichezea Inter Miami CF kwenye mchezo wa Ligi Kuu Marekani (MLS) dhidi ya Philadelphia Union.
Messi mwenye umri wa miaka 38 alionekana kushika nyuma ya mguu wake wa kushoto kabla ya kuomba kutolewa katika dakika ya 73 ya mchezo huo uliochezwa mjini Miami.
Hata hivyo, kocha wa Inter Miami, Guillermo Hoyos, amesema uamuzi wa kumtoa ulikuwa wa tahadhari kutokana na hali mbaya ya uwanja uliokuwa na unyevunyevu mwingi kufuatia mvua.
“Kwa sasa hatujapata taarifa rasmi ya madaktari, lakini alikuwa amechoka sana. Uwanja ulikuwa mzito na hatukutaka kuhatarisha afya yake,” alisema Hoyos baada ya mchezo huo.
Messi ambaye aliiongoza Argentina kutwaa ubingwa wa 2022 FIFA World Cup bado hajatangaza rasmi kama atacheza Kombe la Dunia lijalo, lakini anatarajiwa kuwepo katika kikosi hicho kitakachoshiriki michuano itakayoanza Juni 11 nchini Marekani, Canada na Mexico.
Iwapo atashiriki, Messi ataweka rekodi ya kucheza Kombe la Dunia mara sita, akilingana na idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya mashindano hayo.
Kikosi cha Argentina kinatarajiwa kutangazwa wiki ijayo kabla ya mchezo wao wa kwanza dhidi ya Algeria utakaochezwa Juni 16.
Tangu ajiunge na Inter Miami mwaka 2023, Messi amekuwa akisimamiwa kwa karibu kuhusu kiwango cha michezo anachocheza kutokana na changamoto za majeraha ya misuli ya nyuma ya paja ambazo zimekuwa zikimsumbua mara kwa mara.



