World Cup

Tanzania na nafasi Kombe la Dunia

UKITAJA Kombe la Dunia Tanzania ni taifa la chini ambalo bado halijawahi kufuzu katika fainali hizo kubwa za soka.

Lakini kadiri miaka inavyosogea kuna kitu kinaonekana, kuna mabadiliko ya kimapinduzi yameanza kuonekana.

Soka la nchi linaanza kukua, tayari kuna historia ndogo imeandikwa kwamba nchi imefuzu mara tatu fainali za Mataifa ya Afrika au Afcon. Watu wanaichukulia Tanzania kama taifa dogo kisoka kulingana na historia yake, lakini lolote linawezekana kuanzia sasa na  wakaishangaza dunia.

Katika fainali zijazo zitakazofanyika mwaka 2026, nchini Canada, Marekani na Mexico, kampeni za kusaka nafasi zinaanza kwa Tanzania leo ambapo itacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Niger ugenini nchini Morocco.

Kisha watacheza mchezo wa pili wa Kundi E dhidi ya Morocco Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Katika kundi hilo, kuna Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Morocco.

Ukiacha Morocco ambao walifika nusu fainali za michuano hiyo iliyofanyika nchini Qatar, hao wengine Tanzania inaweza ikawamudu kama wachezaji wataamua kwa kuonesha kiwango bora kushindana na wengine kwenye timu hizo.

KWANINI INAWEZEKANA
Ilitangazwa hivi karibuni uwakilishi wa mataifa ya Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia umeongezeka kutoka matano hadi tisa mpaka 10. Kwa maana hiyo, Tanzania kama nchi ikikazana inaweza kuwa miongoni mwa mataifa 10 ya kuwalisha Bara la Afrika kwenye michuano hiyo.

SABABU
Sababu kuna wachezaji wengi wazuri wanaocheza soka la kulipwa Ulaya na tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na serikali wameanza kuwatafuta
wachezaji hao ili warudi nyumbani kutumikia taifa lao.

Kinachokwamisha wengi kushindwa kuja kuitumikia Tanzania ni uraia. Lakini serikali
kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo hivi karibuni iliweka bayana kuwa kuna
umuhimu wa kutafuta njia za kuwaita wachezaji hao kuja kutumikia nchi.

Mpaka kusema hivyo, huenda sasa wakaangalia uwezekano wa kufanya maboresho ya sheria itakayoruhusu wachezaji kupata uraia wa nchi mbili ili wapate nafasi ya kuja
kutumikia taifa lao lakini pia, kuendelea kucheza soka la kulipwa katika mataifa wanayoishi.

Ukiacha wale wanaojulikana kama akina Mbwana Samatta na wengine nchi imeanza
kampeni ya kuwarejesha mmoja mmoja kujiunga na wale waliozoeleka katika soka la nyumbani ili kufanya vizuri.

Hii ina maana kwamba Tanzania ikifanikiwa kuwarejesha, kutakuwa na timu bora itakayoshindana na mataifa mengine yaliyofanikiwa. Ubora wa timu nyingi za Afrika ukiangalia Morocco, Senegal, Comoro na mataifa mengine asilimia 97 ya vikosi vyao ni wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.

Tanzania asilimia 90 ya wachezaji wa Timu ya Taifa wanacheza soka la nyumbani na baadhi yao wanacheza nje kwa maana ya Ligi za Afrika na wengine Ulaya.

Kocha Mkuu, Adel Amrouche amekuwa akizungumzia umuhimu wa wachezaji hao katika kampeni hizi na tayari katika kikosi kinachotarajia kuchuana na Niger na Morocco kuna sura mpya kadhaa zimeitwa kusaidia.

Huu ni mwanzo mzuri na kwa uhakika wachezaji hao wakichanganywa na wengine wanaweza kuonesha kitu na kusaidia timu kutimiza malengo.

WAPINZANI
Wapinzani wa kwanza ni Niger ambao tayari ilikutana na Tanzania katika michezo ya kufuzu fainali za Afrika. Katika mchezo uliochezwa ugenini Tanzania ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Niger kisha nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikashinda bao 1-0.

Niger si wapinzani wa kubezwa, wana wachezaji wazuri na wazoefu kama ilivyo kwa Tanzania. Pengine wanaweza kuleta upinzani kwa sababu tayari walishakutana lakini
haimaanishi kwamba waogopwe bali waheshimiwe na timu ijipange vizuri zaidi dhidi yao.

Kama wachezaji watacheza kwa kujitolea hakika wanaweza kuondoka na matokeo mazuri.
Kwa upande wa Morocco, ni timu ngumu na nzuri yenye mafanikio makubwa na ina kikosi cha wachezaji wengi wanaocheza soka nchi mbalimbali za Ulaya.

Lakini mpira ni mchezo wa ajabu na kuna wakati una matokeo ya kikatili. Ni kwa namna gani Tanzania itajipanga inaweza kupata matokeo mazuri kama itawaheshimu na  utoogopa
majina na timu pinzani, bali kuzingatia maelekezo ya kocha.

MUHIMU
Timu inahitaji matokeo mazuri kwa kila mchezo kwa kuanza na hizo mechi mbili. Sababu kubwa ni kulinda ile heshima ambayo nchi imepewa ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2027.

Lakini lingine, hii ni fursa kwa wachezaji wazawa watakaopata nafasi kwenye kikosi cha
kwanza. Waoneshe ni kwanini wamechaguliwa wao na si wengine.

Ni nafasi ya kuonesha uwezo wa wachezaji kwa kuamini kuwa wapo wenye ndoto za kutoka, ikiwa wataonesha kile ambacho wanacho pengine kuisaidia timu na kupata mafanikio utakuwa mwanzo wa wao kuonekana na kujiuza kwa mawakala.

MASHABIKI
Katika kampeni hizi mashabiki ni watu muhimu kuiunga mkono timu ya taifa kwa sababu
wakishinda sifa zitakuja kwa Watanzania wote. Mashabiki wajifunze kujikubali licha ya kutofautiana uwezo, wakubali cha kwao kwamba kinaweza.

Na kwenda uwanjani wa matokeo ya aina tatu. Hata kama timu itafungwa wajifunze kuwatia moyo kusudi kuongeza juhudi zaidi. Kila mmoja akitimiza wajibu wake kila kitu kinawezekana na historia mpya itaandikwa.

Related Articles

Back to top button