Maxi, Yao Koussi kuwakosa Al Hilal

DAR ES SALAAM: WACHEZAJI wawili wa Yanga, Max Nzengeli na Yao Koussi hawatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kinachoondoka kesho kuelekea Mauritania katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal.
Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema kwa ushauri wa daktari wa timu hiyo kuwa nyota hao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha msafara huo kwa kuwa hawako fiti kucheza mchezo huo wa ushindani.
Kamwe amesema maandalizi chini ya Kocha Sead Ramovic yanaendelea vizuri kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Al Hilal na malengo yao ikiwa ni kutafuta alama muhimu.
“Wachezaji wote wapo vizuri, habari njema ni kurejea kwa kiungo Clatous Chama na ameanza mazoezi na atakuwa sehemu ya msafara lakini Nzengeli, Yao na Aziz Andambwile hawatakuwa kwenye mipango ya mchezo huo,” amesema.
Yanga watakuwa ugenini katika mchezo wa marudiano dhidi ya Al Hilal katika uwanja wa La Capitale nchini Mauritania.