FA

Max Nzengeli: Yanga tupo vitani

hatuna muda wa kupoteza

DAR ES SALAAM: Baada ya kuifungia Yanga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Coastal Union, nyota wa Yanga, Max Nzengeli, amefichua mambo mawili yanayowapa presha kubwa katika harakati zao za kutetea mataji ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Yanga ilionesha ubora mkubwa, huku ikithibitisha dhamira yao ya kusaka mafanikio makubwa msimu huu.

Ushindi huo uliwahakikishia nafasi ya kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, jambo linalowafanya waendelee kuwa na ratiba ngumu mbele yao.

Max alieleza kuwa kila mechi ni vita mpya kwao, kwani wanahitaji kupambana kwa nguvu zote si tu kwa ajili ya mashabiki wao, bali pia kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kutetea mataji yao yote mawili.

“Kwa sasa hatuna muda wa kupumzika au kusubiri chochote. Tunajua tuna mashindano mawili makubwa yanayotuhitaji kuwa bora kila wakati. Ushindani ni mkubwa, lakini tuna dhamira ya kuhakikisha tunashinda yote,” alisema Max.

Kiungo huyo pia alisisitiza kuwa msaada kutoka kwa mashabiki wa Yanga umekuwa chachu kubwa ya mafanikio yao, kwani wanajitokeza kwa wingi kila wanapocheza, jambo linalowapa motisha ya kupambana zaidi uwanjani.

“Tuna imani kubwa na kikosi chetu. Morali tuliyonayo ni kubwa sana, hasa kutokana na sapoti kutoka kwa mashabiki wetu ambao hawaachi kutuunga mkono popote tunapocheza. Tunawaomba waendelee kuwa nasi mpaka mwisho wa msimu,” aliongeza Max.

Kwa sasa, Yanga inaendelea na maandalizi kwa ajili ya michezo yao ijayo, huku ikisaka kuendeleza rekodi yao nzuri katika mashindano yote mawili.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button