Masanja: Waimbaji wa Injili washirikiane na wasanii wakubwa

DAR ES SALAAM: MSANII wa vichekesho na Mchungaji wa Feel Free Church, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’ Mkandamizaji, amewataka wanamuziki wa injili kuendelea kushirikiana na wasanii wa Bongo Fleva, akisema ushirikiano huo unaweza kuimarisha umoja na upendo miongoni mwa wasanii bila kujali aina ya muziki wanaoufanya.
Masanja amesema hana tatizo na mwanamuziki wa injili Joel Lwaga kushirikiana na staa wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnumz, katika wimbo wao wa Nikumbuke.
Amesema anatamani kuona ushirikiano huo ukiongezeka kwa kuwahusisha wasanii wengine wakubwa wa Bongo Fleva, akiwemo Ali Kiba na Mbosso, ili kuendeleza mshikamano kati ya wanamuziki wa injili na wale wa muziki wa kawaida.
Kauli ya Masanja imekuja kufuatia mjadala ulioibuka baada ya kutolewa kwa wimbo wa Nikumbuke, ambapo baadhi ya watu walionyesha kutoridhishwa na kitendo cha wasanii wa muziki wa injili kushirikiana na wasanii wanaofanya muziki wa kidunia.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki kupitia mitandao ya kijamii wameunga mkono ushirikiano huo, wakieleza kuwa muziki unaweza kuwa daraja la kuunganisha watu na kuhimiza upendo, umoja na kuheshimiana licha ya tofauti za mitazamo na aina za muziki.
Wimbo wa Nikumbuke umeendelea kupata mwitikio kutoka kwa mashabiki kwenye majukwaa mbalimbali ya kidijitali, huku ushirikiano wa Joel Lwaga na Diamond Platnumz ukiibua mjadala kuhusu nafasi ya muziki katika kuunganisha hadhira zenye mitazamo tofauti.
Kwa kauli yake, Masanja anaonekana kuhimiza kufunguliwa kwa milango zaidi ya ushirikiano kati ya wasanii wa injili na Bongo Fleva, akitarajia kuona majina makubwa kama Ali Kiba na Mbosso yakishiriki katika miradi hiyo.




