Manchester United wamsikilizia Pochettino kurejesha makali ya timu

ENGLAND: MANCHESTER United inatarajia kumteua kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur na Paris Saint-Germain, Mauricio Pochettino, kuwa kocha wake mpya baada ya kufikia makubaliano ya awali ya mdomo Jumatano.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari. Hatua hiyo inatarajiwa kumaliza kipindi chake cha miaka miwili akiwa kocha wa timu ya taifa ya Marekani.
Uteuzi huo unakuja wakati United ikiwa katika kipindi kigumu baada ya kuanza msimu vibaya zaidi katika kipindi cha miaka 40. Tangu Sir Alex Ferguson astaafu mwaka 2013, klabu hiyo imepitia makocha 11 bila kutwaa tena taji la Ligi Kuu England.
Pochettino anatajwa kuwa na uwezo wa kujenga upya timu kupitia soka la kasi, presha kubwa kwa wapinzani na kukuza vipaji vya vijana.
Akiwa Tottenham, aliifikisha timu hiyo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019, huku akisaidia kukuza nyota kama Harry Kane.
Kane amekiri kuwa Pochettino alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya maisha yake ya soka, akieleza kuwa kocha huyo alimsaidia kukua ndani na nje ya uwanja. United pia ina vijana wenye vipaji kama Kobbie Mainoo, Leny Yoro na Shea Lacey ambao wanaweza kunufaika na falsafa yake.
Hata hivyo, uteuzi huo una changamoto zake kutokana na vipindi visivyokuwa na mafanikio makubwa alivyopitia Paris Saint-Germain na Chelsea. Pia amekuwa akikabiliwa na ukosoaji kutokana na kushindwa kutwaa mataji mengi makubwa, licha ya kufika fainali tano katika kazi yake ya ukocha.
Akiwa na Marekani, Pochettino aliiongoza timu hiyo hadi hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia lililofanyika nyumbani, huku ikipata ushindi muhimu dhidi ya Paraguay na kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya mtoano tangu mwaka 2002.
Kwa kumteua kocha huyo mwenye umri wa miaka 54, Manchester United inaweka matumaini ya kurejesha utambulisho, mshikamano na ushindani wa timu hiyo, ingawa bado haijathibitisha rasmi uteuzi wake.




