Yanga wanataka kuizoea hali ya hewa Zanzibar

ZANZIBAR: YANGA imeweka kambi maalumu ya siku 10 Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikilenga kuwazoesha wachezaji mazingira na hali ya hewa ya visiwani humo kabla ya kuanza kutumia Uwanja wa New Amaan kwa mechi zake za nyumbani.
Daktari wa timu hiyo, Moses Etutu, ameeleza umuhimu wa maandalizi hayo katika kuwajenga wachezaji kimwili na kuwazoesha mazingira ya Zanzibar, ambayo yatakuwa sehemu ya safari yao ya mashindano ya kimataifa.
Yanga inatarajia kutumia Uwanja wa New Amaan kwa mechi zake za nyumbani katika hatua ya makundi, ikianza na mchezo dhidi ya MC Alger ya Algeria, Novemba 28, hivyo kambi hiyo inatoa nafasi kwa wachezaji kuzoea mazingira kabla ya michezo hiyo.
“Tunataka kuwazoesha wachezaji wetu hali ya hewa ya Zanzibar kwasababu muda sio mrefu tutakuwa hapa kwa mechi zetu za Ligi ya Mabingwa Afrika,”amesema.
Hata hivyo, suala la majeruhi limeendelea kuwa sehemu ya changamoto zinazofuatiliwa na benchi la ufundi, huku kiungo Maxi Nzengeli akiwa miongoni mwa wachezaji wanaofanyiwa matibabu jijini Dar es Salaam baada ya kupata jeraha la goti katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar.
Kwa upande wa kiungo Duke Abuya, aliyepata jeraha la nyama za paja katika dabi dhidi ya Simba, anaendelea vizuri kwa mujibu wa Daktari huyo. Wachezaji wengine waliorejea ni
beki Yao Attohoula na beki Dickson Job.




