Kwingineko

Blatter amshambulia Infantino

USWISI: ALIYEKUWA rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Sepp Blatter, amemshambulia mrithi wake Gianni Infantino, akimtaja kama dikteta na kudai anahitaji msaada wa kitaalamu wa kisaikolojia.

Kauli hiyo aliitoa katika mahojiano na jarida la Ujerumani la Der Spiegel yaliyochapishwa jana Jumatano akidai kwamba hajazungumza na Infantino tangu mwanzoni mwa mwaka 2016.

Blatter mwenye umri wa miaka 90, alikosoa uamuzi wa Infantino kuanzisha tuzo ya Amani ya FIFA na kumkabidhi Rais wa Marekani, Donald Trump, kuelekea Kombe la Dunia la lililoandaliwa na Marekani, Canada na Mexico.

Alisema tuzo hiyo ilikuwa ya aibu kutokana na hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran.

Pia alikosoa mpango wa Infantino wa kuuza sehemu ya haki za kibiashara za Kombe la Dunia katika siku zijazo, ambao ulisitishwa baada ya kupata upinzani mkubwa.

Blatter alidai Infantino anatumia ahadi za kuongeza fedha kwa mashirikisho ya soka ya mataifa mbalimbali ili kupata uungwaji mkono katika uchaguzi wa urais wa FIFA.

Aliongeza kuwa baadhi ya watu ndani ya taasisi hiyo wanamwona Infantino kama kiongozi asiyepaswa kuguswa.

Blatter aliongoza FIFA kuanzia mwaka 1998 hadi alipojiuzulu mwaka 2015 kufuatia tuhuma za rushwa. Ingawa alikabiliwa na mashtaka, baadaye aliachiliwa katika kesi mbili, lakini akafungiwa kushiriki shughuli za soka na kamati ya maadili ya FIFA.

Pia alikosoa uamuzi wa FIFA wa kufuta kadi nyekundu aliyopewa mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, akisema sheria za mchezo zinapaswa kutumika kwa usawa bila kujali ushawishi wa mtu yeyote.

Wakati huohuo, Blatter amemtaja rais wa Shirikisho la Riadha Duniani, Sebastian Coe, kuwa mtu anayefaa kuiongoza FIFA, huku Kozo Tashima wa Japan naye akitangaza nia ya kuwania urais.

Related Articles

Back to top button