Ahmed: Masharti ya CAF yanatuumiza Simba

DAR ES SALAAM: WAKATI Simba ikijiandaa kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mashabiki wa klabu hiyo wamekumbana na changamoto ya idadi ndogo ya watazamaji watakaoruhusiwa kuingia Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuweka ukomo wa mashabiki 6,000 pekee.
Uamuzi huo umewasikitisha Wanasimba wengi kutokana na idadi kubwa ya mashabiki wanaotaka kuishuhudia timu yao katika mechi za nyumbani, hasa ikizingatiwa ukubwa wa wapinzani wanaosubiriwa katika Kundi C, wakiwamo Orlando Pirates ya Afrika Kusini na RS Berkane ya Morocco.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa klabu imepata ruhusa ya kutumia Uwanja wa Uhuru kwa mechi zake za hatua ya makundi, lakini CAF imeweka ukomo huo kutokana na hali ya miundombinu ya uwanja tofauti na natarajio yao walitamani Uwanja ujae.
Ahmed amesema licha ya kizuizi hicho, klabu itatoa utaratibu maalumu wa upatikanaji wa tiketi ili mashabiki watakaopata nafasi waweze kuingia uwanjani kuisapoti timu yao.
Hata hivyo, Simba inaingia katika hatua hiyo ikiwa na dhamira ya kulipa kisasi dhidi ya wapinzani wake wawili, RS Berkane na Orlando Pirates, ambao waliwahi kuizima ndoto yake ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na kufika hatua ya nusu fainali katika misimu iliyopita.
Kwa upande wa RS Berkane, Simba inakumbuka kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, huku Orlando Pirates ikiwa na kumbukumbu ya kuiondoa timu hiyo kwa mikwaju ya penalti katika robo fainali ya mashindano hayo msimu wa 2021/22.
Ahmed Ally amesema Simba imejipanga kutumia nafasi hiyo kuonesha ushindani tofauti, akisisitiza kuwa kikosi kina uwezo wa kufanya vizuri iwapo wachezaji watatimiza majukumu yao kwa asilimia 100.
Katika maandalizi, Ahmed amesema wachezaji wameanza kurejea kambini na kuendelea na mazoezi, huku kikosi kikiendelea kujipanga kwa mechi za Ligi Kuu na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inalenga kuanza vizuri kampeni yake ya Kundi C, ikitarajia kuwakabili Orlando Pirates katika mchezo wa kwanza wa nyumbani mwishoni mwa Novemba, kabla ya kuendelea na mikikimikiki ya kundi hilo dhidi ya RS Berkane na Colombe Sportive ya Cameroon.
Kwa ujumla, Wekundu wa Msimbazi wanataka kutumia michuano hiyo kurekebisha makosa ya misimu iliyopita na kupambana kufika hatua ya juu zaidi, huku wakihitaji sapoti ya mashabiki wao licha ya nafasi chache zitakazopatikana Uwanja wa Uhuru.




