Kwingineko

De la Fuente ana matumaini Yamal ataikabili England

HISPANIA: KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Luis de la Fuente, amesema ana matumaini mshambuliaji kinda wa Barcelona, Lamine Yamal, atakuwa fiti kuikabili England katika mchezo wa Ligi ya Mataifa Ulaya (UEFA Nations League) utakaopigwa mwishoni mwa wiki.

Yamal mwenye umri wa miaka 19, ataukosa mchezo wa Hispania dhidi ya Jamhuri ya Czech utakaochezwa Alhamisi mjini Prague kutokana na tatizo la goti, lakini anatarajiwa kujiunga na kikosi cha timu hiyo baada ya mchezo huo.

Nyota huyo alicheza katika ushindi wa mabao 2-1 wa Barcelona dhidi ya Atletico Madrid kwenye Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) Jumapili iliyopita. Hata hivyo, Jumatatu Hispania ilitangaza kuwa mchezaji huyo hatasafiri na kikosi kwenda kukutana na Czech.

Akizungumza na waandishi wa habari, De la Fuente alisema Yamal alipata maumivu ya goti katika mchezo uliopita na vipimo vilivyofanyika Barcelona vilibaini kuwepo kwa uvimbe na majimaji kwenye goti hilo, hali iliyomlazimu kupumzika.

Kocha huyo alisema alishauriana na madaktari wa timu ya taifa pamoja na wale wa Barcelona na kuamua kutomhusisha Yamal katika safari ya Prague hadi pale atakapokuwa amerejea katika hali nzuri ya kucheza.

Hata hivyo, De la Fuente amesema amezungumza na mshambuliaji huyo na ana matumaini makubwa kuhusu maendeleo ya kupona kwake kabla ya mchezo dhidi ya England utakaochezwa Madrid Jumapili.

Alisema Yamal anaendelea na mazoezi maalumu ya kurejesha hali yake chini ya uangalizi wa wataalamu wa tiba wa klabu yake na anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Hispania Ijumaa.

Kocha huyo pia alikanusha madai kuwa Yamal anapewa upendeleo maalumu ndani ya kikosi cha Hispania licha ya umaarufu wake, akisisitiza kuwa wachezaji wote wanatendewa kwa usawa.

Wakati huohuo, Hispania tayari imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mataifa Ulaya baada ya kushinda michezo yote minne ya Kundi A3.

Timu hiyo haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake 43 za mashindano rasmi, rekodi ambayo De la Fuente amesema inawapa hamasa ya kuendelea kuweka alama mpya katika historia ya soka.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button