Ligi Daraja La Kwanza

Simple:Nandy alitaka Helikopta kabla ya nyumba, nimezuia

DAR ES SALAAM: MENEJA wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Faustina Mfinanga ‘Nandy’, anayefahamika kwa jina la Simple The Boy, amefichua kuwa msanii huyo aliwahi kuwa na mpango wa kununua helikopta kabla ya kuamua kununua nyumba, lakini alimshauri kusubiri hadi watakapofikia kiwango hicho.

Simple The Boy amesema uamuzi wa kumzuia Nandy kununua helikopta ulitokana na maoni yake binafsi, akibainisha kuwa si familia ya msanii huyo wala mume wake waliohusika katika kumshawishi kubadili uamuzi huo.

Akisimulia tukio hilo, meneja huyo amesema “Nandy alimweleza kuwa alitaka kujizawadia helikopta kutokana na changamoto alizokuwa akikutana nazo katika masuala ya usafiri.

“Nandy aliniambia anataka kununua helikopta kwa sababu anataka kujizawadia, lakini pia huwa anapata tabu kwenye masuala ya usafiri.

“Nilimuuliza kwa nini anataka kununua helikopta, nikamshauri kuwa bado hatujafikia kiwango hicho na atafute kitu kingine kizuri,” amesema Simple The Boy.

Ameongeza kuwa baada ya mazungumzo hayo, Nandy alikuja na wazo la kununua nyumba ambayo alikuwa ameiona na kuipenda kila alipokuwa akiitazama.

“Nandy alikuja kuniambia, ‘Hii nyumba kila ninapoiangalia nazidi kuipenda, acha ninunue.’ Nikamwambia sawa, kwa sababu nyumba ni kitu kinachoweza kupanda thamani kadiri muda unavyokwenda,” ameeleza.

Simple The Boy amesema Nandy amekuwa akifanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya majengo, akidai kuwa mwanamuziki huyo ana nyumba nyingi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ikiwemo mikoani na Zanzibar.

Kauli hiyo inaonesha namna Nandy anavyofikiria kuhusu zawadi binafsi na uwekezaji, huku uamuzi wa kununua nyumba ukionekana kuwa chaguo aliloliona linafaa zaidi kwa wakati huo.

Related Articles

Back to top button