Chapo aahidi kumaliza pambano mapema

DAR ES SALAAM: Bondia Mohamed Chapo wa Masaki amemjibu mpinzani wake Bakari Kibiki maarufu kama Simba wa Kigamboni, akiahidi kumaliza pambano lao kabla halijafika mwisho katika tamasha la Dar Boxing Derby litakalofanyika Julai 24, 2026 Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akiendelea na maandalizi yake, Chapo amesema amesikia maneno na tambo za mpinzani wake, lakini anaamini hazitabadilisha matokeo ya pambano hilo.
Amesema Simba wa Kigamboni anapaswa kutambua kuwa anakwenda kukutana na bondia mwenye uwezo mkubwa zaidi na kusisitiza kuwa mpinzani wake hataimaliza raundi ya nne kutokana na kipigo atakachopata.
Kocha wa Chapo, Issa Alfan, amesema : “maandalizi yamekamilika na bondia yuko tayari kuonesha kiwango bora na kuibuka na ushindi,
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa na mapambano mengine makubwa yakiwemo ya Juma Choki dhidi ya Tonny Rashid, Dulla Mbabe dhidi ya Hussein Itaba, Haidary Mchanjo dhidi ya Oscar Richard, Hamad Furahisha dhidi ya John Patrick wa Tegeta.
Kwa upande wa wanawake, Debora Mwenda atazichapa na Dorothea Mhoza, huku Sara Alex akitarajiwa kupambana na Dorisia Mazige katika mapambano yanayotarajiwa kuongeza ushindani kwenye tamasha hilo.




