Hamisa Mobetto: Bima iliokoa gari langu baada ya ajali

DAR ES SALAAM: Mwanamitindo, Hamisa Mobetto, amesema huduma ya bima ilimsaidia kuepuka hasara baada ya gari lake kupata ajali.
Hamisa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutangazwa rasmi kuwa balozi wa kampeni ya “Upo Salama”.
Amesema kama asingekuwa na bima, angelazimika kutumia fedha nyingi kutengeneza gari lake.
“Nilipata ajali iliyosababishwa na kijana wa chuo aliyekuwa amelewa. Bahati nzuri nilikuwa na bima, hivyo ilinisaidia kutengeneza gari langu. Kama nisingekuwa na bima, ningepata hasara kubwa zaidi,” amesema Hamisa.
Aidha, ameishukuru CRDB Insurance kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwa balozi wa kampeni hiyo, akieleza kuwa ni heshima kubwa kwake.
“Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii na wote walioniamini. Nitajitahidi kutekeleza wajibu wangu ipasavyo. Mimi pia ni mtumiaji wa huduma za bima, hivyo ninaelewa umuhimu wake na naamini ndiyo sababu nimechaguliwa kuwa balozi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance, Wilson Mnzava, amesema kampuni imeanzisha kampeni ya “Upo Salama” kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda mali na kupunguza athari za hasara zinazoweza kujitokeza.
Amesema Hamisa Mobetto atakuwa balozi wa kampeni hiyo kwa kipindi cha miezi sita, akitarajiwa kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kuwa na bima kwa ajili ya kulinda mali na maisha yao.




